Licha ya majeshi ya Kenya kudai yametwaa maeneo mji wa Kismayo, msemaji wa kundi la Al-Shabab kwenye mji huo amekanusha wapiganaji wake kushindwa na kudai kuwa mapigano bado yanaendelea umbali wa maili 9 toka mji wa Kismayo.
Mwishoni mwa juma majeshi ya Kenya yalishambulia uwanja wa ndege wa Kismayo ambao umekuwa ukitumiwa na wapiganaji wa Al-Shabab na kufanikiwa kuwafurusha toka kwenye uwanja huo na kurudi nyuma.
Kwenye operesheni hiyo kumeripotiwa watu kadhaa kupoteza masiah huku wengine wakijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya anga na yale ya ardhini yaliyotekelezwa na wanajeshi wa Kenya.
Mji wa Kismayo ndio umekuwa ngome ya mwisho ya wapiganaji wa kundi la Al-Shabab ambao walivokimbia toka mjini Mogadishu walipiga kambi kwenye mji huo wakidai ndio mji wao.
Majeshi ya Kenya kwa kushirikiana na majeshi ya AMISOM na vikosi vya Serikali ya Somalia yamekuwa yakifanya operesheni za pamoja katika kukabiliana na wapiganaji hao mjini Mogadishu na maeneo mengine ambayo walikuwa wanayakalia.