Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amesema anajisikia mwenye furaha kwa juhudi za rais Obama kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Cuba. Carter ameiita hatua hiyo ya mabadiliko ya sera kuwa ya kishupavu. Carter anapuuzia shutuma kuwa rais Barack Obama anawafurahisha viongozi wa kikomunist wa Cuba., kama anavyosema seneta wa chama cha Republican Marco Rubio.
Amesema leo kuwa njia sahihi ya kuleta demokrasia kwa Wacuba ni kuwaruhusu Wamarekani kwenda nchini humo kufanya biashara na kuwekeza.
Carter alijaribu kurejesha uhusiano na Cuba muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka 1977, kwa kuanzisha ubalozi wa Marekani na kujadili kuachiliwa huru kwa maelfu ya wafungwa.
Wakati huo huo kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis amesifu hatua ndogo za kidiplomasia zinazofikiwa ambazo zimeleta mahusiano bora kati ya Marekani na Cuba.