Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejiripua na kuwaua watu wanne na kuwajeruhi wengine kiasi ya 48 katika kituo cha basi jimboni Potiskum kaskazini mwa Nigeria. Afisa mmoja wa polisi aliyefika katika eneo la mkasa amesema miili ya waliouawa na waliojeruhiwa imeondolewa. Mhudumu wa afya wa hospitali kuu ya Potiskum pia amethibitisha idadi ya waathiriwa na kuongeza jamaa zao wamefika hospitalini kuwatafuta wapendwa wao. Mji huo umeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi wa kundi la Boko Haram ambao wamewaua kiasi ya watu 13,000 na kusababisha wengine milioni moja unusu kuyatoroka makaazi yao kaskazini mwa Nigeria. Nchi jirani na Nigeria, Cameroon, Niger na Chad zinashrikiana kwa pamoja kuunda kikosi cha pamoja cha kijeshi kukabiliana na kitisho cha Boko Haram ambacho kimevuka mipaka.