Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir ameonya dhidi ya kujenga uadui mpya kuhusiana na Uislamu. Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tunis, Steinmeir amesema iwe katika bara la Ulaya au ulimwengu wa Kiarabu majibu ya kujitowa katika hali hiyo ni rahisi. Mwanasiasa huyo wa chama cha SPD nchini Ujerumani wakati huo huo ameushajiisha ulimwengu wa Kiarabu kuchukuwa hatua zaidi kuelekea kwenye demokrasia.Tunisia ni kituo cha pili cha ziara yake ya siku nne kwa mataifa ya Afrika kaskazini ambapo kwanza aliizuru Morocco.Waziri huyo anatarajiwa kukamilisha ziara yake nchini Algeria mwishoni mwa juma ambapo amepangiwa kukutana na Rais Abdelaziz Bouteflika na Waziri Mkuu Abdelmalek Sellal.
Wakati hayo yanaendelea Mwenyekiti wa baraza la waislamu nchini Ujerumani Aiman Mazyek, amesema matumizi ya nguvu dhidi ya waislamu na maeneo yao ya kuabudu yanaongezeka. Kwenye ripoti yake katika jarida la mtandaoni hii leo Aiman Mazyek amesema matusi dhidi ya wasilamu hasa kwa wanawake waliovaa hijabu, uharibifu wa misikiti na vurugu dhidi ya maimamu yamekuwa mambo yanayofanyika kila siku nchini Ujerumani. Mazyek amelilaumu vuguvugu la Pegida linalowapinga waislamu kwa kuongezeka kwa vurugu hizo. Hata hivyo vuguvugu hilo limesema linapinga matumizi ya nguvu ya Waislamu walio na itikadi kali na kukanusha madai ya kwamba wanawapinga Waislamu waliojumuikka katika jamii au kuwa ni wabaguzi. Vuguvugu hilo la PEGIDA limekuwa likiandaa maandamano ya kila wiki mjini Dresden kwa miezi kadhaa sasa yaliowavutia waandamanaji 25,000. Aidha Mazyek amesema baraza lake linashindwa kukabiliana na idadi kubwa ya vijana wa kiislamu nchini Ujerumani wanaojiunga na makundi ya waislamu walio na itikadi kali. Mwenyekiti huyo amesema wanahitaji juhudi zao kuungwa mkono na jamii pamoja na wanasiasa.