Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya, wamekubaliana kuiwekea Urusi vikwazo vipya kutokana na madai ya kujihusisha kwake katika mgogoro wa Ukraine. Mratibu wa sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya Federica Mogherini aliwaambia waandishi habari kwamba yeye pamoja na mawaziri wa mambo ya nchi za nje 28 wa Umoja huo, wamekubaliana kuandaa orodha mpya ya watu watakaokabiliwa na vikwazo hivyo, katika kipindi cha wiki ijayo. Bibi Mogherini alisema uamuzi wa mwisho kutekeleza vikwazo hivyo ambavyo ni pamoja na kuzuiwa mali na kuwapiga marufuku watakaokuwemo katika orodha hiyo,kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya, utachukuliwa kwenye mkutano mwingine wa mawaziri hao Februari 9.
Wakati huo huo kiongozi wa zamani wa uliokuwa Umoja wa Kisovieti Mikhail Gorbachev ameonya kwamba kitisho cha vikwazo zaidi kinaifanya hali mpya ya vita baridi, igeuke mgogoro mkubwa wa kijeshi baina ya Urusi na nchi za magharibi unaoweza kuiyumbisha dunia.