Makombora ya angani ya Marekani yamemuuwa mhandisi wa silaha za kemikali, Abu Malik ambae pia aliwahi kufanya kazi chini ya Saddam Hussein, katika utengenezaji wa silaha hizo. Kwa mujibu wa taatifa za Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Abu Malik aliuwawa Januari 24 katika operesheni ya pamoja karibu na eneo la Mosul, Iraq.
Malik alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza silaha za kemikali cha Muthana kabla ya kujiunga na al-Qaeda mwaka 2005 nchini Iraq ambapo baadae alijiunga na kundi la kigaidi la Daesh. Taarifa ya wizara hiyo iliongeza kusema kwamba kifo chake kinatarajiwa kusambaratisha kwa muda mtandao huo wa kigaidi na kupunguza uwezo wake kuunda silaha za kimekili.
Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Marekani anaemaliza muda wake Chuck Hagel amesema huenda Marekani ikalazimika kupeleka nchini Iraq vikosi vya ardhini kusaidia kulirudisha nyuma kundi la kigaidi la Daesh. Hata hivyo Hagel amesema vikosi hivyo sio vya kushiriki katika mapigano.
Kiongozi huyo ambae alitangaza kujiuzulu kwake kutokana na shinikizo mwezi Novemba mwaka jana alikiambia kituo cha televisheni cha CNN kwamba juhudi zote hazina budi kuchukuliwa nchini Iraq, ikiwemo kutuma vikosi hivyo vya ardhini ambavyo jukumu lake litakuwa kutafuta taarifa za kijasusi na kubainisha maeneo ya kimkakati ya magaidi wa Daesh.
Wanajeshi hao watakuwa nyongeza ya wengine waliopo nchini Iraq 4,500, ambao wanajihusisha na majukumu ya mafunzo na ushauri.