Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al Moallem ameishutumu nchi jirani ya Jordan kwa kufanya mashambulizi ya angani nchini humo dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la kigaidi la Daesh. Al Moallem amewaambia wanahabari hii leo kuwa nchi yake haihitaji msaada wa kutoka nje kupambana na wanamgambo hao wa Daesh, na hiataruhusu Jordan wala nchi nyingine kuingiza majeshi yake nchini Syria kupambana na magaidi wa Daesh na iwapo itafanya hivyo, itachukulika kama ukiukaji wa haki ya kujitawala ya Syria. Hata hivyo Jordan imeapa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya magaidi wa Daesh baada ya mmoja wa marubani wake kuuawa na wanamgambo hao. Al Moallem ameishutumu pia Jordan kwa kuruhusu magaidi akiashiria wapiganaji wanaopinga serikali kuingia nchini humo.
Jordan ni moja kati ya nchi ya nchi zilikuwa zikitoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi yanayotaka kuiangusha serikali ya Syria.
Na huko Iraq kiasi ya watu 22 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad hii leo siku moja tu baada ya serikali kuondoa marufuku ya kutotoka nje usiku iliyowekwa mjini humo kwa zaidi ya muongo mmoja. Waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi aliifuta marufuku hiyo hapo jana ambayo imekuweko tangu mwaka 2004. Katika shambulizi la kwanza, mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejiripua katika kituo cha kusubiri magari nyakati za asubuhi ambapo watu wengi hukusanyika kuelekea makazini na kuwaua watu 18. Takriban watu wengine 42 wamejeruhiwa katika kisa hicho, saa chache baadaye bomu liliripuka katika eneo la kibiashara katika mtaa wa Husseiniyah na kuwaua raia wanne na kuwajeruhi wengine tisa.
Kwa upande wa Yemen vyama viwili vimejiondoa katika mazungumzo yanayosimamiwa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa Jamal Benomar yaliyoanza tena hii leo kuutatua mzozo wa kisiasa wa Yemen baada ya kusema vimepokea vitisho kutoka kwa waasi wa kundi la Houthi. Chama kikuu ya cha upinzani nchini Yemen Islah na chama kidogo cha kisiasa cha Nasserist vimejiondoa kutoka duru ya kwanza ya mazungumzo hayo yaliyoanza leo vikisema vimetishiwa na mwakilishi wa Houthi Mehdi al Mashaat. Mzozo huo wa Yemen unahofiwa huenda ukasababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuyapa nguvu makundi ya kigaidi baada ya waasi wa Houthi kunyakua madaraka, kulivunja bunge na kusitisha katiba baada ya kujiuzulu kwa Rais Abed Rabbu Mansour Hadi na baraza lake la mawaziri mwezi uliopita.