Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh lijiitalo Dola la Kiislamu, wanaripotiwa kulihamisha kundi la mateka wao wa jamii ya Kikristo nchini Syria kwenye ngome yao ya Mto Khabur, mpakani mwa Uturuki na Iraq. Siku ya Jumatatu, Daesh iliwateka wanavijiji 70, Wakristo wa madhehebu makongwe ya Assyria, na hadi sasa hatima ya mateka hao haijuilikani. Marekani, ambayo inaongoza kampeni ya kimataifa ya kijeshi dhidi ya kundi hilo la kigaidi, imelaani vikali kutekwa kwa wanavijiji hao. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Bernadette Meehan, amesema hivi leo kwamba utekaji nyara huo ni miongoni mwa matukio ya kikatili yanayofanywa na kundi la kigaidi la Daesh dhidi ya raia. Kuna taarifa kwamba kundi la kigaidi la Daesh imewateka pia watu wapatao 100, wakiwemo watoto, kwenye mji wa Tikrit, nchini Iraq. kundi la kigaidi la Daesh linawatuhumu mateka hao wa Tikrit, ambao ni Wasunni, kwa kushirikiana na maadui dhidi yake.