Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana limeshutumu kile ilichokieleza kuwa ni vitendo vya kinyama vya kigaidi nchini Iraq vinavyofanywa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh, ikiwa ni pamoja na kuharibu sanaa za kidini na za utamaduni. Video iliyotolewa na kundi hilo la itikadi kali la magaidi wa Daesh siku ya Alhamis zinaonesha watu wakivunja sanamu la kale la Assiria na masanamu mengine ya kuchonga , baadhi yake ni ya karne ya 7 kabla ya kuzaliwa Yesu, kwa nyundo na mashine za kutobolea, wakisema ni vitu vya ushirikina.Baraza la Usalama limesema katika taarifa kuwa limeshutumu vikali unyama huo unaoendelea nchini Iraq unaofanywa na kundi la kigaidi la Daesh.
Wakati huo huo kundi la maseneta wa vyama vya Democratic na Republican nchini Marekani wamewasilisha sheria jana ambayo itahitaji kupitiwa na baraza la Congress iwapo makubaliano yoyote ambayo utawala wa rais Obama na mataifa mengine yenye nguvu duniani yatafikiwa na Iran kuhusiana na mpango wake wa kinyuklia. Hatua hiyo inataka kwamba rais Barack Obama awasilishe waraka wa makubaliano yoyote kwa bunge na unaizuwia serikali hiyo kusitisha vikwazo vya bunge la Marekani dhidi ya Iran kwa siku 60. Katika wakati huo , bunge litasikiliza na kupata fursa ya kuidhinisha , ama kukataa ama kutochukua hatua yoyote katika makubaliano hayo.Sheria hiyo ni changamoto mpya kwa mamlaka ya rais Obama wakati Marekani na mataifa mengine yanazungumza na Jamhuri ya kiislamu Iran kuhusiana na uwezo wake wa kinyuklia. Huenda lakini ikalazimu rais Obama kutumia uwezo wake wa kura ya turufu.