Maelfu ya watu wameandama katikati mwa mji mkuu wa Urusi, Moscow kutoa heshima zao kwa kiongozi wa upinzani Boris Nemtsov, aliyepigwa risasi na kuuwa karibu na ikulu ya rais ya Kremlin Ijumaa iliyopita. Umati mkubwa wa waandamanaji waliobeba bendera za Urusi na picha za Nemtsov waliandamana kutoka uwanja wa Moscow hadi katika daraja ambako Nemtsov alipigwa risasi mgongoni muda mfupi baada ya saa sita usiku Ijumaa iliyopita, huku wakimtaka rais wa Urusi Vladimir Putin ajiuzulu. Katika maandamano yaliyoonekana kuwa makubwa tangu maandamano ya kuupinga utawala wa Kremlin mnamo mwaka 2011 hadi 2012 kuwavutia zaidi ya watu 100,000, waandamanaji walimuenzi Nemtsov huku wakiishutumu Urusi kwa msimamo wake kuhusu Ukraine. Nemtsov aliyewahi kuwa naibu waziri mkuu wa Urusi na mkosoaji mkubwa wa rais Putin atangu aliporejea madarakani mwaka 2000, ni mwanasiasa wa ngazi ya juu kuuwawa nchini Urusi tangu kusambaratika kwa muungano wa zamani wa Sovieti. Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limetaka mauaji hayo yachunguzwe kwa makini.
Wakati huo huo Korea kaskazini imefyetua makombora mawili baharini na kuapa kuchukua hatua kali bila huruma huku Marekani na Korea Kusini zikianza mazeozi ya pamoja ya kijeshi. Korea Kaskazini imeyakosoa mazoezi hayo ikiyataja kuwa uchokozi na imeonya huenda ikalisukuma eneo la Korea katika ukingo wa vita. Jeshi la Korea Kusini limesema makombora mawili ya Korea Kaskazini yalifyetuliwa kutoka mji wa bandari wa Nampo magharibi ya Korea Kaskazini na kuvuka nchi hiyo kabla kuanguka baharini katika pwani ya mashariki.