18 Machi 2015 - 10:11
Jeshi la Nigeria lasema limewafurusha Boko Haram

Jeshi la Nigeria limesema limewafurusha waasi wa kundi la Boko Haram kutoka maeneo yote isipokuwa matatu tu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo

Jeshi la Nigeria limesema limewafurusha waasi wa kundi la Boko Haram kutoka maeneo yote isipokuwa matatu tu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kudai ushindi baada ya kampeini kabambe ya kupambana na waasi wao huku taifa hilo likitarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu tarehe 28 mwezi huu. Jeshi la Nigeria limepigwa jeki katika kampeini yake ya kukabiliana na waasi hao baada ya kupata usaidizi kutoka kwa majeshi ya Chad, Niger na Cameroon. Mnadhimu mkuu wa jeshi la Nigeria, Luteni Jenerali Tobia Minimah amesema maeneo yanayosalia kukombolewa ni Abadam, Kala Balge na Gwoza. Minimah pia amesema mpaka sasa hawajapata taarifa kuwahusu zaidi ya wasichana mia mbili wa shule waliotekwa nyara na Boko Haram miezi kumi na moja iliyopita.