Waziri mkuu wa Italia Mateo Renzi amesema nchi yake inafanyakazi pamoja na Malta kuwaokoa wahamiaji ambao wamo katika maboti mawili yaliyo katika hatari ya kuzama katika bahari ya Meditterrania.
Shirika la kimataifa la kuwahudumia wahamiaji IOM, limepokea taarifa kuhusu boti nyingine iliyowachukua wahamiaji ambayo imezama baharini na kwamba watu 20 wamefariki katika ajali hiyo ya hivi karibuni kabisa.
Mtu ambaye hakutambuliwa amepiga simu katika ofisi ya shirika hilo , mjini Rome akisema wamo katika boti ambayo inazama ikiwa na watu 300, ikiwa ni pamoja na watu 20 ambao tayari wamefariki. Mtu huyo pia amesema kuna maboti matatu yakiwa katika hali ya hatari. Meya wa mji wa Catania nchini Italia Enzo Bianco amesema amejisikia uchungu kwa watu wengi kupoteza maisha.
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameyaambia mataifa wanachama leo hawana visingizio vingine vya kutochukua hatua kuhusu mzozo wa wahamiaji.
Mogherini amesema hayo wakati akiwasili katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani na mambo ya kigeni ulioitishwa na waziri mkuu wa Italia Mateo Renzi kuzungumzia suala hilo.