Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Majesi yamekuwa katika hali ya tahadhari huku Maelfu ya watu wakiandamana katikati mwa mji mkuu wa Algeria, Algiers, kupinga hatua ya Rais Abdelaziz Bouteflika kuendelea kung'ang'ania madarakani. Maandamano hayo yameanza baada ya swala ya Ijumaa, huku vikosi vya usalama vikiangalia bila kuyaingilia maandamano hayo. Waandamanaji wanapinga hatua ya Bouteflika kugombea urais kwa muhula wa 5 kutokana afya yake kuwa mbaya. Wakati huo huo, wabunge kadhaa wa chama tawala nchini Algeria cha FLN, wamejiuzulu na kuungana na waandamanaji wanaoipinga serikali. Taarifa hizo zimetangazwa leo na kituo binafsi cha televisheni cha Ashourouq. Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi ambazo zimetolewa kuhusu hilo. Bouteflika ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1999, amekuwa akiugua kiharusi tangu mwaka 2013. Tangu mwezi uliopita kiongozi huyo amelazwa katika hospitali moja nchini Uswisi kwa kile ambacho serikali imekieleza kuwa ni kwa ajili ya kuangaliwa afya yake.
Mwisho wa habari/ 291