11 Juni 2019 - 09:20
Hatua ya tatu ya serikali ya Trump; Ukingo wa Magharibi baada ya Quds na Golan

David Friedman, balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amedai kuwa Israel ina haki ya kutwaa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

(ABNA24.com) David Friedman, balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amedai kuwa Israel ina haki ya kutwaa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Tangu mwezi Disemba 2017 hadi hivi sasa, msimamo wa serikali ya Donald Trump huko Marekani ni kuikandamiza zaidi na zaidi Palestina katika mgogoro wake na Israel hususan katika masuala ya ardhi. Tarehe sita Disemba 2017, rais wa Marekani, Donald Trump alichukua uamuzi ulio kinyume na sheria wa kuitangaza Quds kuwa eti ni mji mkuu mpya wa utawala pandikizi wa Israel na mwezi Mei 2018 alihamishia mjini Quds, ubalozi wa Marekani uliokuweko Tel Aviv.

Katika hatua ya baadaye ya mwezi Machi 2019, Trump alidai kuwa milima ya Golan ya Syria eti ni mali ya utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo alitangaza kulitambua rasmi jambo hilo. Katika kujibu hatua hiyo ya kichokozi ya Trump, Syria ilisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kuishambulia moja kwa moja ardhi ya Syria kwani milima ya Golan ni sehemu isiyotenganishika na ardhi nyingine za nchi hiyo ya Kiarabu.

Hivi sasa na katika hatua ya tatu, serikali ya Trump inadai kuwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni haki ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisema baada ya Trump kutangaza rasmi kuwa milima ya Golan ya Syria ni mali ya Israel kwamba, kitendo cha ulimwengu wa Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu cha kunyamazia kimya hatua hiyo ya Trump, basi watu wanapaswa kusubiri kuona hatua nyingine mbaya ya Trump ambapo sasa atasema, Ukingo wa Magharibi nao ni ardhi ya Israel na huu hapa Muamala wa Karne. 

Takriban miezi miwili tu tangu Sayyid Hassan Nasrullah alipotoa utabiri huo, balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amejitokeza na kudai kuwa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni mali ya Israel. Miezi miwili iliyopita, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni wa Israel aliahidi kuviunganisha na Israel vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Wiki iliyopita na katika kumbukumbu ya vita vya siku 52 huko Ghaza, Netanyahu alisema kuwa, Israel itaendelea kuzikalia milele ardhi ilizoziteka, tena basi aliutaja kwa jina Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Kwa kweli hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi rasmi wa Marekani kutangaza waziwazi kuwa Israel ina haki ya kumiliki baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Maamuzi ya Marekani na matamshi ya Netanyahu yamekumbwa na upinzani mkali ndani ya Marekani kati ya makundi ya Israel na baina ya makundi ya Palestina. 

Wiki iliyopita, maseneta kadhaa wa Marekani waliwasilisha muswada katika Baraza la Sanate la nchi hiyo kupinga hatua za serikali ya Donald Trump zilizo dhidi ya Wapalestina kama vile jaribio la kutaka kuipa Israel ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Harakati ya Israel ya mrengo wa kushoto inayojulikana kwa jina la Amani Sasa imemtaka Donald Trump amfute kazi balozi wake David Friedman kutokana na matamshi yake kuhusu kumilikiwa na Israel Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Makundi ya Palestina nayo yamelaani vikali matamshi hayo ya balozi wa Marekani na kusema kuwa huo ni ushahidi wa wazi wa ubeberu wa dola hilo la kiistikbari.

Mwisho tunapenda kusema kuwa, matamshi ya balozi huyo wa Marekani kuhusu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yametolewa katika hali ambayo maazimio ya kimataifa yanazihesabu ardhi za Palestina zilizotekwa kuanzia mwaka 1967 ukiwemo mji wa Quds na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni sehemu ya ardhi ya Paelsina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni na kwamba Israel haina haki yoyote katika ardhi hizo na haina ruhusa za kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni wala kitu kingine chochote kwani ni ardhi unazozikalia kwa mabavu.




/129