17 Juni 2019 - 10:29
Njia za utatuzi za Rais Vladmir Putin kwa ajili ya mapatano ya JCPOA

Hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka jana na pia ukiukaji wa ahadi wa mara kwa mara wa Umoja wa Ulaya ambao umeshindwa kulinda mapatano hayo kupitia kuanzisha mfumo utakaosaidia kupunguza athari hasi za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, ni mambo yaliyoyaweka katika hali mbaya mapatano hayo.

(ABNA24.com) Hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka jana na pia ukiukaji wa ahadi wa mara kwa mara wa Umoja wa Ulaya ambao umeshindwa kulinda mapatano hayo kupitia kuanzisha mfumo utakaosaidia kupunguza athari hasi za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, ni mambo yaliyoyaweka katika hali mbaya mapatano hayo.

Suala hilo ndilo lililozusha wasi wasi mkubwa wa serikali ya Russia. Rais Vladmir Putin wa Russia siku ya Jumamosi alisema katika kikao cha tano cha Kundi la Maingiliano na Hatua za Kujenga Imani Barani Asia (CICA) kuwa: "Moscow inaamini kwamba kuendelea kuheshimiwa mapatano ya JCPOA, ndiyo njia ya utatuzi wa mgogoro uliopo kuhusu mapatano hayo." Ukweli ni kwamba Rais wa Russia anaamini kuwa, kitendo cha Washington cha kukataa kuendelea kutekeleza ahadi zake ndani ya mapatano hayo na pia hatua zake hasi dhidi ya JCPOA, hususan hatua ya serikali ya Trump ya kuiwekea tena vikwazo vya nyuklia Tehran, ndiyo sababu ya hali kuzidi kuwa mbaya. Kwa ajili hiyo ili kuhitimisha mgogoro uliozushwa ndani ya mapatano hayo, ni jambo la dharura kufanya juhudi za kuyalinda si tu kupitia kuitaka Marekani kurejea kwenye makubaliano hayo, bali pia pande za Ulaya nazo hususan troika ya nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, zinatakiwa kutekeleza haraka iwezekanavyo ahadi zao kwa Iran na kuacha kukwamisha mambo.

Hata Moscow pia inasisitizia udharura wa kutekelezwa ahadi katika mapatano hayo. Rais Vladmir Putin sambamba na kubainisha kwamba, anaamini kuwa utekelezwaji wa mapatano hayo ndiyo njia sahihi, amesisitiza kwamba Moscow itatekeleza kikamilifu mapatano hayo ya JCPOA. Aidha tarehe 14 mwezi huu wa Juni na katika kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai SCO huko Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan, Rais Putin sambamba na kusisitizia ulazima na umuhimu wa kulindwa na kutekelezwa mapatano hayo alisema: "Nchi zote wahusika wa mapatano ya JCPOA zinalazimikiwa kutekeleza ahadi zao katika fremu ya mapatano hayo na tunafanya juhudi kubwa katika uwanja huo." Sisitizo la Rais wa Russia juu ya udharura wa kulindwa mapatano ya JCPOA na kuendelea kutekelezwa kwake, sambamba na kuzingatia msimamo mkuu wa dola hilo lenye nguvu kimataifa na ambalo ni mshindani wa Marekani, limetokana na nafasi muhimu ya mapatano hayo ya nyuklia ya JCPOA. Russia kama mmoja wa madola yenye nguvu ambayo ina mitazamo mingi inayokinzana na Marekani, imechukua msimamo sawa na mataifa ya Ulaya katika uwanja huo. Kwa mtazamo wa wajumbe wa kundi la 4+1, kuyavuruga mapatano ya JCPOA au kuyavunja, kutakuwa na taathira hasi kwa usalama wa kimataifa. Hii ni kusema kuwa, Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni mapatano ya pande kadhaa ambayo yanaweza kuwa kigezo na aina bora ya utatuzi wa mizozo ya kimataifa.

Kwa mtazamo wa Russia, mwenendo wa Marekani kuhusu Iran, uko kinyume kikamilifu na misingi na sheria za kimataifa na unahatarisha usalama na amani ya eneo la Asia Magharibi na dunia nzima kwa ujumla. Aidha Moscow inaamini kwamba, mienendo hiyo hasi ya Washington kuihusu Tehran inazidisha hatari ya kuzuka vita. Lakini kinyume kabisa na matakwa ya Marekani na misimamo yake ya upande mmoja ambayo daima imekuwa ikipigia ngoma ya kutaka kufutwa mapatano hayo na kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Iran ya Kiislamu, lakini kwa upande wake jamii ya kimataifa ikiwemo Russia, inataka kulindwa mapatano hayo. Katika mazingira ya hivi sasa, hatua za Marekani dhidi ya mapatano hayo na misimamo kinzani ya Ulaya na kutotekeleza ahadi zao kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya nyuklia vya Washington dhidi ya Iran, ni mambo yaliyoifanya Tehran ilazimika kuchukua hatua maalumu kama za kupunguzwa utekelezaji wa ahadi zake ndani ya makubaliano hayo kwa kutegemea vipengee vya 26 na 36 vya JCPOA. Suala hilo lilitahadharishwa pia na Russia. Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alipozngumzia suala la je mapatano hayo yako katika njia ya kusambaratika taratibu au la amesema: "Hivi sasa mapatano ya JCPOA yako chini ya uangalizi maalumu." Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, iwapo wanachama wa kundi la 4+! hawatochukua hatua athirifu na za haraka za kulinda mapatano hayo, basi kubakia kwake kutakuwa hatarini.



/129