7 Julai 2019 - 05:26
Baraza la Usalama lataka vita visitishwe nchini Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa rasmi na kutaka vita visitishwe nchini Libya na pande mbili kurejea katika meza ya mazungumzo.

(ABNA24.com) Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa rasmi na kutaka vita visitishwe nchini Libya na pande mbili kurejea katika meza ya mazungumzo.

Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, pande mbili hasimu zinapaswa kusitisha vita na kurejea katika meza ya mazungumzo ili kuandaa uwanja wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Kadhalika taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imelaani vikali shambulio la hivii karibuni dhidi ya eneo linalohifadhiwa wahajiri jirani na mji mkuu Tripoli ambalo lilipelekea makumi ya wahajiri wasio na hatia kuuawa.

Taarifa hiyo inatolewa katika hali ambayo, Ghassan Salame, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataiifa katika masuala ya Libya hivi karibuni alitoa wito kama huo wa kusitishwa vita nchini Libya.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahajiri limetangaza kuwa, karibu watu 1000 wameshauawa tangu jenerali muasi Khalifa Haftar alipoanzisha mashambulio dhidi ya mji kuu wa Libya Tripoli, mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Jenerali Khalifa Haftar ambaye anaongoza vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya anaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na Ufaransa na anashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya.

Mashirika mbalimbali ya kieneo na kimataifa ya misaada ya kibinadamu yameendelea kuonya kuhusiana na kuzidi kuzorota hali ya kibinadamu katika nchi hiyo.




/129