8 Julai 2019 - 07:48
ICC kutoa hukumu dhidi ya 'Terminator' Ntaganda wa DRC leo

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inatazamiwa kutoa hukumu dhidi ya kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bosco Ntaganda, ambaye anaandamwa na mashitaka 13 ya jinai za kivita na matano ya uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Ituri, mashariki mwa DRC.

(ABNA24.com)  Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inatazamiwa kutoa hukumu dhidi ya kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bosco Ntaganda, ambaye anaandamwa na mashitaka 13 ya jinai za kivita na matano ya uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Ituri, mashariki mwa DRC.

ICC imesema itasoma hukumu dhidi ya Ntaganda leo Jumatatu (Julai 8) katika kikao cha hadhara kitakafofanyika mjini The Hague nchini Uholanzi.

Ntaganda anatuhuma kutumia watoto kama wapiganaji vitani na kuwatumia mateka wa kike kama watumwa wa ngono. Agosti mwaka jana,  alidai mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuwa yeye si mhalifu bali ni mwanamapinduzi.

Ntaganda ambaye ni mashuhuri kwa jina la "The Terminator" au Muangamizaji, alishitakiwa kwamba wapiganaji wa kundi lake waliua na kunajisi raia wakati kundi hilo lilipovamia eneo lenye utajiri wa madini ya dhahabu la Ituri kuanzia mwaka 2002 hadi 2003.

Bosco Ntaganda Septemba mwaka 2015 alikanusha tuhuma 13 za kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na kundi lake la FPLC la wanamgambo wa kabila la Hema dhidi ya watu wa jamii ya Lendu na jamii nyingine.

Iwapo atapatikana na hatia basi atafungwa miaka 30 jela huku baadhi ya weledi wakisema Ntaganda atafadhilisha kufungwa katika gereza lolote la nchi ya Ulaya kuliko kukamatwa na kufungwa jela Rwanda au DRC.



/129