17 Julai 2019 - 05:36
Uturuki kuendelea na mpango wa kuchimba mafuta na gesi Bahari ya Mediterania licha ya upinzani wa EU

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesisitiza kuwa, nchi hiyo itaendelea na mpango wake wa kutafuta mafuta na gesi mashariki ya bahari ya Mediterania licha ya agizo la Umoja wa Ulaya kuitaka isimamishe mpango huo.

(ABNA24.com) Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeeleza kuwa, maamuzi ya Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo hayataathiri kwa namna yoyote ile azma ya Ankara ya kuendeleza shughuli zake za kutaka kuchimba mafuta na gesi katika eneo la mashariki ya bahari ya Mediterania na pwani ya Cyprus.

Taarifa hiyo aidha imebainisha kuwa, kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wa Cyprus kunategemea hakikisho la kupatiwa haki zao raia wa kisiwa hicho wenye asili ya Uturuki na ikaongeza kwamba, kama ilivyokuwa huko nyuma, Uturuki itaendelea kupigania kwa nguvu zote haki zake na za Wacyprus wenye asili ya Uturuki.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wametoa taarifa maalumu mwishoni kwa kikao chao kilichofanyika mjini Brussels wakisisitiza kuwa, shughuli za Uturuki za utafutaji rasilimali za nishati mashariki ya Mediterania zinafanyika kinyume cha sheria na kubainisha kwamba EU itapitisha maamuzi kadhaa dhidi ya Ankara.

Katika miaka ya karibuni, suala la utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Cyprus limekuwa na umuhimu mkubwa kwa Uturuki, kiasi kwamba hatua ilizochukua nchi hiyo katika uwanja huo zimezusha hitilafu kubwa kati yake na Umoja wa Ulaya.../



/129