(ABNA24.com) Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika kikao cha pande mbili kilichofanyika jana usiku hapa mjini Tehran kati ya Iran na ujumbe wa ngazi ya juu wa Iraq ulioongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Adil Abdul-Mahdi.
Ameeleza kuwa, kustawishwa uhusiano na ushirikiano kati ya Iran na Iraq katika wakati huu kuna umuhimu na akaongezea kwa kusema: Katika mazingira ambayo uthabiti na usalama unaohitajika bado haujarejea katika eneo, hakuna shaka kuwa kustawishwa ushirikiano na uhusiano wa pande zote kati ya Tehran na Baghdad kutakuwa na taathira chanya katika kuimarisha amani na uthabiti wa eneo hili.
Rais Rouhani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipendelei kuona mivutano inaongezeka katika eneo wala kuwa na mivutano na nchi zingine za eneo hili na wala haitakuwa mwanzishaji vita na mivutano; na akafafanua kwa kusema: Katika zama zote za historia Iran imekuwa na itaendelea kuwa mlindaji mkuu wa amani na mdhamini wa kufanyika kwa uhuru safari za majini katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz na Bahari ya Oman.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq Adil Abdul-Mahdi, amesema udugu na urafiki ni hisia za pande mbili zilizoko baina ya Iran na Iraq.
Amefafanua kwa kusema, safari iliyofanywa na Rais Rouhani nchini Iraq ilikuwa ya kihistoria na nukta muhimu sana katika uhusiano wa Tehran na Baghdad na akaashiria makubaliano muhimu yaliyofikiwa kati ya nchi mbili katika safari hiyo kwa kusema: Viongozi wa wa nchi mbili wanaupa uzito na umuhimu utekelezaji wa makubaliano hayo; na Iraq inaahidi kutekeleza masuala iliyoafikiana na Iran.
Aidha ameashiria baadhi ya njama zinazofanywa ili kuzidisha mivutano na hali ya wasiwasi katika eneo na akasisitiza kuwa, Iraq katu haijawahi kuwa na wala haitakuwa miongoni mwa watekelezaji vikwazo dhid ya Iran.../
/129
23 Julai 2019 - 08:21
Msimbo wa Habari: 963748
Rais Hassan Rouhani amesema, hatua athirifu zingali zinaendelea kuchukuliwa katika kupanua na kustawisha uhusiano wa pande zote kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.