(ABNA24.com) Baraza la Taifa la Palestina limetangaza kuwa, kusitishwa utekelezaji wa hati za makubaliano yaliyofikiwa kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Israel ni mwanzo wa awamu mpya ya makabiliano ya pande zote na Wazayuni maghasibu.
Salim Az-Zaanun, mkuu wa Baraza la Taifa la Palestina amesema, baraza hilo linaubebesha dhima utawala ghasibu wa Kizayuni na serikali ya rais Donald Trump wa Marekani ya sera na hatua zote za kihasama zinazochukuliwa dhidi ya Wapalestina.
Baraza hilo aidha limeyataka makundi na mirengo yote ya Palestina kuiunga mkono Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika kipindi hiki nyeti na hasasi.
Wakati huo huo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa, uamuzi wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kusitisha utekelezaji wa makubaliano iliyofikia mamlaka hiyo na utawala wa Kizayuni ni hatua inayofuata mkondo sahihi.
Abbas ametangaza kuwa: Baada ya kubomolewa nyumba za Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi, maafikiano yote ambayo Mamlaka ya Ndani ya Palestina imefikia na utawala wa Kizayuni yatasimamishwa kwa muda usiojulikana.
Siku ya Jumatatu iliyopita, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulitenda jinai ya kubomoa makumi ya nyumba za Wapalestina karibu na mji wa Baitul Muqaddas kwa madai ya kujengwa kinyume cha sheria.../
/129