(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani ameashriia vikwazo chungu nzima vinavyowekwa katika uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi, ongezeko la kila uchao la umasikini, kukosekana usalama, uhajiri na kupungua ukuaji wa uchumi duniani na akasisitiza kwa kusema: Mfumo wa Kimataifa unahitaji mashirikiano ya kiuchumi ya baina ya pande kadhaa na ya kikanda.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa sisitizo hilo siku ya Jumanne katika kikao cha viongozi wa Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia (Eurasian Economic Union) unaojumuisha nchi za Asia na Ulaya Mashariki, kilichofanyika Yerevan, mji mkuu wa Armenia.
Amesema kusainiwa hati ya makubaliano ya kibiashara kati ya Iran na Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia kunadhihirisha mtazamo mpana, chanya na uliokamilika wa Tehran, sambamba na irada madhubuti ya kisiasa ya kusaidia kustawishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa baina ya pande kadhaa na wa kikanda.
Rais Rouhani ameitaka jamii ya kimataifa ichukue uamuzi madhubuti na hatua athirifu za kukabiliana na mielekeo ya kihasama na ya kujichukulia hatua za upande mmoja ya Marekani; na akafafanua kwa kusema: Katika miaka ya karibuni, kwa kuchukua hatua za upande mmoja, kwa kutojali majukumu yake na makubaliano ya kimataifa, sambamba na kukiuka mikataba ya pande mbili, Marekani imechukua hatua za kuzilenga nchi nyingi ikiwemo China na Russia na hata waitifaki wake kadhaa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Hatua za mabavu za Marekani na kuitumia sarafu ya dola kama silaha vitaishia kwenye ugaidi wa kiuchumi na kuyaathiri maisha ya raia wa kawaida.
Dakta Rouhani aidha amebainisha kuwa, ushrikiano wa pamoja na wa kikanda kupitia miungano ya kiuchumi, kibiashara na kisiasa ukiwemo Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO), Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na Baraza la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) ni nyenzo muhimu za mashirkiano ya pamoja ya kiuchumi na kisiasa ya kikanda yanayoungwa mkono na Iran.../
/129