(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye amefanya safari huko Japan kufuatia mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abe Shinzo jana Ijumaa alikutana na kuzungumza naye kuhusu uhusiano wa pande mbili na masuala mengine muhimu ya kieneo na kimataifa.
Weledi wengi wa mambo wameitathmini ziara hii katika fremu ya kupanuliwa uhusiano kati ya Iran na Japan. Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Japan ameeleza kufurahishwa na safari ya Rais wa Iran ya kuitembelea nchi hiyo na kusisitiza kuwa nchi yake ina hamu ya kuimarisha uhusiano na Iran katika nyanja zote. Katika uga wa kisiasa pia; mazungumzo ya Rouhani na Abe Shinzo yalikuwa na umuhimu kwa kuzingatia mitazamo ya pamoja ya nchi mbili kuhusu usalama katika eneo, suala la makubaliano ya JCPOA na kadhia ya nyuklia.
Katika mazungumzo na Abe Shinzo, Hassan Rouhani amebainisha hivi kuhusu makubaliano ya JCPOA: Iran imefanya kila jitihada ili kuyalinda makubaliano hayo katika fremu ya kudhamini maslahi yake na itaendelea kufanya hivyo. Amesema kuwa Iran imechukua hatua za kupunguza uwajibikaji wake ndani ya makubaliano ya JCPOA marhala kwa marhala baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo na nchi za Ulaya kutochukua hatua yoyote ya kutekeleza ahadi zao kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano hayo ya nyuklia.
Kuhusu usalama wa eneo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha pia kuwa Tehran siku zote imekuwa ikifanya juhudi za kudhamini amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi na ulimwenguni kwa ujumla kwa msaada na ushirikiano na nchi za eneo na jirani; na imetuma pia barua kwa wakuu wa nchi za eneo hili kuhusu suala hilo. Kitendo cha kukiuka makubaliano ya JCPOA na vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya Iran ni hatua inayokinzana na sheria za kimataifa na siasa kuu za uchukuaji maamuzi za nchi kama Japan, China, Russia na Umoja wa Ulaya; na ni hatua inayokwenda kinyume pia na misingi na kanuni za biashara huru ya kimataifa. Kwa msingi huo, tunaweza kuelewa ni kwa nini Japan inatiwa wasiwasi na hali ilivyo katika makubaliano ya JCPOA na kuendelea mvutano katika eneo kwa sababu mwenendo huu umekuwa na taathira hasi kwa uthabiti wa uchumi wa aghalabu ya nchi ikiwemo Japan.
Zaidi ya asilimia 80 ya vyanzo vya nishati ya Japan vinapitia katika lango Bahari la Hormoz; na ukwamishaji mdogo kabisa katika mchakato wa kudhamini vyanzo hivyo tajwa utaigharimu pakubwa nchi hiyo tajiri kwa viwanda. Japan ni nchi ya tatu yenye uchumi mkubwa duniani, na ni nchi ya tatu inayonunua kwa wingi mafuta kutoka nje baada ya Marekani na China. Kwa msingi huo, Japan haiwezi kupuuza soko la nishati la Iran.
Katika uchambuzi wake, gazeti la Japan Times limeeleza kuwa katika mazingira haya ni jambo muhimu sana na lenye manufaa ikiwa nchi isiyoegemea upande wowote kama Japan itachukua hatua kuhusiana na suala hilo.
Jambo lililo wazi ni kuwa, hatua na misimamo ya upande mmoja ya Marekani hadi sasa imeisababishia madhara makubwa jamii ya kimataifa. Kama alivyoeleza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo na Abe Shinzo, mzizi wa hali ya mchafuko katika eneo inapasa ung'olewe. Katika miaka miwili iliyopita Trump hajasita kuchukua hatua yoyote ambayo kwa imani ya Marekani ingeweza kutoa pigo kwa makubaliano ya JCPOA au kuzuia maendeleo ya Iran.
Kama alivyoeleza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kinyume cha sheria kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA si tu kuwa haijawa na maslahi kwa Marekani yenyewe wala upande wowote wa mapatano hayo ya kimataifa; bali imethibitisha kuwa vikwazo havina matokeo mengine isipokuwa madhara kwa pande zote.
Japan ni nchi ambayo imeonyesha katika siasa zake kwamba inaheshimu na kufuata kanuni zinazotawala katika uhusiano wa kimataifa. Kwa msingi huo, inatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzo, atabaini vyema vitisho halisi katika eneo na kimataifa; na kufanya juhudi za kuimarisha usalama endelevu katika Asia Magharibi bila ya kufuata siasa za Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alipofanya mazungumzo na Abe Shinzo, Waziri Mkuu wa Japan wakati wa safari yake hapa Tehran mwezi Juni mwaka huu, alieleza yafuatayo kuhusu matamshi ya Shinzo kuhusiana na ombi la Marekani la kufanya mazungumzo ya kujadili kadhia ya nyuklia: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya mazungumzo kwa miaka mitano hadi sita na Marekani na nchi za Ulaya katika kalibu ya kundi la 5+1 kuhusu kadhia ya nyuklia na kufikia natija; lakini Marekani imekiuka makubaliano hayo; na kwa msingi huo ni mtu gani mwenye akili timamu ambaye anaweza kufanya mazungumzo kwa mara ya pili na nchi ambayo inakiuka makubaliano yote?
/129