3 Januari 2020 - 12:52
Rais Rouhani: Kuuliwa shahidi Soleimani kutazidisha azma ya Iran ya kupambana na ubeberu wa Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuuliwa shahidi Meja Jenerali Qassem Solaimani aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi al Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah) kutazidisha mara dufu azma ya Iran na mataifa mengine huru ya kusimama kidete kupambana na ubeberu wa Marekani na kulinda thamani na maadili ya Kiislamu.

(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani amelaani jinai ya Marekani ya kumuua shahidi Qassem Soleimani na wenzake kadhaa hususan mpigana jihadi mkubwa, Abu Mahdi al Muhandes na kusema: Hapana shaka kuwa, taifa la Iran na mataifa mengine huru katika kanda hii yatalipiza kisasi dhidi ya Marekani mtenda jinai.

Rais Rouhani amesema kuwa, kitendo hiki cha kijinai na kiwoga ni kielelezo kingine cha kuchanganyikiwa na udhaifu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na hisia za kuchukiwa utawala huo baina ya mataifa ya eneo hilo; Marekani ambayo imeamua kukanyaga kanuni zote za kibinadamu na sheria za kimataifa na kuzidisha doa jingine la aibu katika ukurasa mbaya wa historia ya nchi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, bendera ya izza na kusimama kidete ya shahidi huyo itaendelea kupeperushwa na askari wengine wengi wa Uislamu na njia yake yenye fahari kubwa ya kujisabilia katika njia ya Allah na mapambano itaendelea mbele kwa nguvu kubwa zaidi.

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) Meja Jenerali Qassem Solaimani na naibu mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hasdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes wameuawa shahidi mapema leo Ijumaa katika shambulizi la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq. 

.........
340