Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

31 Oktoba 2022

19:50:56
1319251

AU na EAC zataka kusitishwa mapigano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kusitishwa mara moja mapigano yanayoongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni Mjumbe wa Umoja huo na Mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mzozo huo, ametaja wasiwasi wake mkubwa juu ya hali huko mashariki mwaCongo na kuzitaka pande zote kuheshimu sheria za kimataifa, usalama wa raia na utulivu katika mipaka ya nchi zote za ukanda huo.

Katika upande mwingine, mwenyekiti wa AU Macky Sall na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wamesema katika taarifa yao kwamba, "wanaelezea wasiwasi wao mkubwa" kutokana na kuzorota kwa usalama na wakaomba utulivu na mazungumzo.

Mwito huo umetolewa masaa machache tu baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumtimua balozi wa Rwanda nchini humo Vincent Karega kufuatia tuhuma za muda mrefu kuwa Kigali inawaunga mkono waasi wa M23. Rwanda, ambayo inakanusha shutuma hizo, imeelezea kusikitishwa na uamuzi huo na kuongeza kuwa wanajeshi wake kwenye mpaka wa nchi hizo mbili wako kwenye tahadhari kubwa.

Mwezi Mei pia, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kidemokeasia ya Congo Kongo ilimwita Karega ili kumuhoji kuhusu madai hayo kuhusu waasi wa M23.

Rais wa Angola Joao Lourenco amesema atamtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje Tete Antonio nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kupatanisha mzozo huo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara kwa mara imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara. Uamuzi wa kumfukuza Karega unatarajiwa kuzua zaidi mvutano kati ya nchi hizo mbili ambazo uhusiano wao umekuwa mgumu kwa miongo kadhaa.

Rwanda ilikariri wasiwasi wake juu ya kile ilichokiita kuendelea kushirikiana kati ya wanajeshi wa Kongo na waasi wa Rwanda wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, wenye makao yake nchini Kongo.

342/