Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

21 Julai 2023

12:38:39
1381035

Magaidi wengine watano wa al Shabab waangamizwa katika shambulio la anga

Magaidi wengine watano wameangamizwa katika shambulio la anga lililofanyika kwenye eneo la Galcad nchini Somalia. Shambulio hilo limekuja baada ya zaidi ya magaidi 100 wa al Shabab kuangamizwa katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa zinasema kwamba shambulizi hilo la anga ni muendelezo wa operesheni za Jeshi la Taifa la Somalia linaloshirikiana na vikosi vya kigeni kupambana na magaidi hao wakufurishaji.

Magaidi wa al Shabab wamejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Somalia imekumbwa na vita na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikuu vya kiusalama vikitoka kwa al Shabab na magenge mengine ya kigaidi kama Daesh yaani ISIS.

Tangu 2007, magaidi wa al Shabab wanapigana na serikali ya Somalia inayosaidiwa na kikosi maalumu cha Umoja wa Afrika ATMIS na Umoja wa Mataifa.

Juzi Jumatano pia, magaidi wasiopungua 100 wa wa al Shabab waliangamizwa katika operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na vikosi vya kigeni katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wizara ya Habari ya Somalia ilisema magaidi hao wa al Shabab waliuawa katika operesheni kabambe iliyofanyika juzi Jumatano katika vijiji vya Gal-Libah na El Quraq vilivyopo katika mpaka wa majimbo ya Galgaduud na Middle Shabelle.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, magaidi hao wakiwemo makamanda wao saba wa ngazi za juu wameuawa katika operesheni ya pamoja ya vikosi vya Somalia kwa ushirikiano na vikosi vya kigeni.

Jumatano hiyo hiyo, Jeshi la Taifa la Somalia lilitangaza habari ya kuangamiza magaidi 30 wa alShabab wakiwemo makamanda wao wawili katika eneo la El Quraq la katikati mwa nchi hiyo.

342/