Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

22 Desemba 2023

19:59:38
1422566

Waziri wa zamani wa utalii Kenya, Najib Balala, afikishwa mahakamani kwa kesi ya ufisadi

Waziri wa zamani wa Utalii katika serikali ya utawala wa Jubilee, Bw Najib Balala, amefikishwa katika Mahakama Kuu ya mji wa Malindi akikabiliwa na kesi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma takriban Shilingi bilioni 8.5 za ujenzi wa chuo cha utalii cha Ronald Ngala katika eneo la Vipingo, Kaunti ya Kilifi.

Balala na wenzake kadhaa, wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwa ni pamoja na ufujaji wa fedha hizo zilitolewa katika hazina ya Tourism Fund kwa minajili ya ujenzi wa chuo hicho.

Balala alikamatwa jijini Nairobi na maafisa wa upelelezi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na kusafirishwa kwa ndege hadi Malindi ili kufikishwa mahakamani.

Waziri huyo wa zamani wa utalii katika Baraza la Mawaziri la Rais Uhuru Kenyatta alikamatwa pamoja na maafisa wengine wa zamani wa wizara hiyo.

Wengine waliokamatwa ni pamoja na; Leah Adda Gwiyo (aliyekuwa katibu wa wizara), Flora Ngina (Aliyekuwa Meneja wa ICT, Mfuko wa Utalii) na Joseph Odero (mhandisi wa West Consult Engineers).

Msemaji huyo wa EACC, Erick Ngumbi amesema wanne hao wamekamatwa kuhusiana na malipo ya Shilingi bilioni 18.5 ambazo zilipaswa kutumiwa kwa ajili ya kujenga chuo hicho huko Kilifi ambacho baadaye kilibadilishwa jina na kuwa Chuo cha Ronald Ngala Utalii.

Kulingana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kukamatwa kwao kunakuja baada ya uchunguzi uliofanywa na Tume kuhusiana na malipo yasiyo ya kawaida ya shilingi bilioni 8.5 yaliyotolewa na Hazina ya Utalii, ambapo shilingi bilioni 4 zililipwa kwa Baseline Architects Limited kwa huduma za ushauri kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Ronald Ngala Utalii huko Vipingo, Kaunti ya Kilifi.

Tume ya Kupambana na Ufisadi ya Kenya imekuwa ikiwafuatilia maafisa wakuu waliohudumu katika Wizara ya Utalii wakati wa utawala wa zamani akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Utalii, Balala na naibu wake.

342/