Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Hojjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Shahrestani, katika kikao na kundi la maafisa wa Kamati Tendaji ya Kongamano la Tano la Kimataifa la Wanaharakati wa Kitamaduni wa Arbaeen, baada ya kueleza riwaya kadhaa kuhusu utukufu wa Arbaeen na mapenzi ya kipekee ya wananchi wa Iraq kwa mazuwaru wa Imam Hussein (a.s), aliongeza kuwa: Ni lazima tukubali kwamba pamoja na huduma zote zinazotolewa, bado hatujalitekeleza ipasavyo haki ya Arbaeen. Mamilioni ya watu kutoka nchi mbalimbali husafiri kwa miguu katika safari hii ndefu, na hili ni tukio kubwa sana. Bila shaka, ni utukufu na heshima ya Sayyid al-Shuhadaa (a.s) unaowaita watu kwenye harakati hii ya kimataifa, na hivyo hutokea tukio lenye ukubwa usio na mfano popote pengine.
Aligusia nafasi na hadhi ya kuwahudumia mazuwaru wa Arbaeen miongoni mwa watu wa Iraq, na akaendelea kusema: Kuwahudumia mazuwaru wa Arbaeen ya Imam Hussein ni fahari kwa wananchi wa Iraq. Wahudumu wa Kiiraqi huweka mezani kila walicho nacho ili kuwahudumia vyema zaidi mazuwaru. Gharama na matumizi wanayotoa hayawezi kupimika, kwani wanafanya yote hayo kwa mapenzi ya Imam wao.
Hojjat al-Islam wal-Muslimin Shahrestani alisema: Ninyi pia mnapaswa kuthamini mapenzi haya ya Husseini, na sasa kwa kuwa mmepewa fursa hii adhimu kama wahudumu wa kitamaduni wa Arbaeen, itumieni kwa njia bora kabisa. Hakika huduma zenu hazitapotea bila malipo.
Aliongeza kuwa: Bila shaka Imam Mahdi (a.f.s) anawashika mkono wahudumu katika njia hii; la sivyo tukio hili kubwa lisingewezekana. Kama tulivyoona katika vita vya siku 12 dhidi ya Iran, Imam wa Zama (a.f.s) alisaidia hadi nguvu ya Iran ikaonekana wazi kwa ulimwengu mzima.
Mwanzoni mwa kikao hicho, Hojjat al-Islam wal-Muslimin Hamid Ahmadi, Mkuu wa Kamati ya Kitamaduni na Kielimu ya Arbaeen, akirejelea ushiriki wa wageni na wasomi 300 kutoka nchi 20 katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Wanaharakati wa Kitamaduni wa Arbaeen, alisisitiza kuwa: Katika kongamano hili la siku tatu, mafanikio muhimu zaidi ya Arbaeen iliyopita yatachunguzwa, na mipango itaandaliwa kwa ajili ya Arbaeen ya mwaka 1405 Hijria Shamsi.
Your Comment