Balozi wa Iran mjini London, Ali Matinfar, amesema leo Jumapili kwamba ubalozi huo umetuma ujumbe wa malalamiko kwa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza baada ya watu wenye chuki kuwanyanyasa washiriki wa duru ya kwanza ya upigaji kura siku ya Ijumaa.
Ameongeza kuwa ujumbe huo pia umesisitiza haja ya kulindwa usalama wa Wairani katika duru ya pili ya uchaguzi huo Ijumaa ijayo.
Matinfar ameongeza kwamba atafuatilia suala hilo kwa karibu katika mikutano yake na maafisa wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza wiki hii.
Mnamo Juni 28, maelfu ya Wairani wanaoishi nchini Uingereza walipiga kura katika vituo 10 vya kupigia kura vilivyowekwa katika miji ya London, Manchester, Birmingham, Newcastle, Glasgow na Cardiff kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa rais wa Iran.Wakati huo huo, wapinzani kadhaa wenye chuki dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran waliandamana nje ya vituo hivyo vya kupigia kura huku wakilaani na kuwatukana wapiga kura. Polisi wa Uingereza waliwakamata wafanyavurugu sita.
Hata hivyo, shughuli ya upigaji kura iliendelea bila kusitishwa ambapo wapiga kura walieleza kuchukizwa kwao na hatua za wafanyavurugu hao wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi.
Zaidi ya watu milioni 24 walipiga kura katika uchaguzi wa Ijumaa ili kumchagua mtu atakayechukua nafasi ya Rais Ebrahim Raisi, ambaye alikufa shahidi katika ajali ya helikopta Mei 19.
Hakuna mmoja kati ya wagombea aliyepata kura zilizohitajika ili kushinda kinyang'anyiro hicho katika duru ya kwanza. Washiriki wawili wa kwanza waliopata kura nyingi zaidi, yaani Masoud Pezeshkian na Said Jalili, watachuana katika duru ya pili ya uchaguzi huo ambayo imepangwa kufanyika Julai 5.
342/