Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

5 Julai 2024

15:29:48
1469802

Muda wa kupiga kura kwenye uchaguzi wa rais Iran warefushwa

Muda wa kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Iran iliyoanza mapema leo kote nchini, umerefushwa kwa saa mbili, hiyo ikiwa na maana kuwa zoezi hili litaendelea hadi saa mbili usiku kwa saa za hapa nchini.

Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Tume ya Uchaguzi nchini Iran, kwa idhini ya Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmed Vahidi, imerefusha muda wa kupiga kura hadi saa mbili usiku kutokana idadi kubwa ya wapigakura.

Ijumaa iliyopita, muda wa kupiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo wa rais ulirefushwa kwa muda wa saa sita, na kwa msingi huo, vituo vya kupigia kura vilifungwa saa sita usiku. Kwa mujibu wa sheria, muda huo hauwezi kurefushwa zaidi ya sita usiku.

Mamilioni ya Wairani tangu mapema leo asubuhi, wamejitokeza kushiriki katika uchaguzi wa rais utakaoainisha kiongozi wa Serikali ya Awamu ya 14 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini hapo mwaka 1979 ambaye atachukua nafasi ya Sayyid Ebrahim Raisi aliyeaga dunia Mei 19 katika ajali ya helikopta.Saeed Jalili, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa na kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na nchi za Magharibi, anachuana na waziri wa zamani wa afya, Daktari Masoud Pezeshkian katika duru hiyo ya pili.

Wawili hawa walipata kura nyingi zaidi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Iran iliyofanyika Ijumaa iliyopita. Tume ya Uchaguzi imetangaza kuwa, iataanza kutoa matokeo ya awali mara tu baada ya kukamilika zoezi la upigaji kura na kuanza kazi ya kuhesabu kura.



342/