Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Julai 2024

15:19:19
1470293

Kiongozi Muadhamu akutana na Rais mteule wa Iran na Jalili

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian na kumpongeza kwa kuibuka mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.

Katika kikao hicho cha jana alasiri, Ayatullah Ali Khamenei sambamba na kumpongeza Rais mteule wa Iran kwa mafanikio ya kupata kura nyingi katika uchaguzi huo wa Ijumaa, ameeleza kuridhishwa kwake na mwenendo mzima unaoongezeka, wa ushiriki wa watu katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Kiongozi Muadhamu amesema anatumai kuwa Rais mteule atatumia uwezo wa watu na rasilimali na uwezo mwingine wa nchi kulilitea ustawi na maendeleo taifa hili.

Aidha jana alasiri, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikutana na kufanya mazungumzo na Saeed Jalili, ambaye alichuana na Pezeshkian katika duru ya pili ya kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu. 

Kiongozi Muadhamu amemshukuru na kumpongeza Jalili kwa kufanya kampeni zilizowatia watu hamasa ya kushiriki katika uchaguzi huo. Aidha amemtakia Jalili ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa na kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na nchi za Magharibi, kheri na fanaka maishani.

Wakati huo huo, Dakta Pezeshkian alikutana na kufanya mazungumzo na Saeed Jalili jana usiku hapa mjini Tehran, ambapo Jalili alimpongeza Rais mteule kwa ushindi wake.

Pezeshkian amesema kuwa mipango pekee haitoshi kuendesha mambo, akisisitiza kuwa watu maalumu na wenye ujuzi wanapaswa kuteuliwa ili kuhakikisha kwamba mipango hiyo inatekelezwa vyema. Kadhalika amesema kuwa yuko tayari kupokea maoni na nasaha za Jalili.

342/