Araghchi amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Micheál Martin jana Jumatatu na kusisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kupunguza mvutano katika eneo hili."
Ameongeza kuwa, Benjamin Netanyahu na utawala wa Kizayuni unaendeleza ghasia na kuzieneza katika maeneo mengine ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran pia amesema kuwa, Tehran itaunga mkono makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yatakayokubaliwa na Wapalestina na harakati ya muqawama ya Hamas.
Duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano, kwa upatanishi wa Misri, Qatar na Marekani, imeanza tena mjini Cairo huku hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza ikizidi kuzorota, utapiamlo unaongezeka na hakuna nukta yoyote ya ukanda huo iliyo salama.
Hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshaua shahidi zaidi ya Wapalestina 40,780 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo huko Ghaza tangu mwezi Oktoba 2023.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland ameonesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka mvutano katika eneo la Asia Magharibi na kusema kuwa nchi yake inatoa mwito wa kusimamishwa vita mara moja huko Ghaza, kubadilishana mateka na kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ghaza.
342/