Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Chicago Council ya nchini Marekani umeonyesha kuwa watu sita kati ya kila watu kumi ambayo ni sawa na asilimia 59 ikiwemo asilimia 73 ya Wademocrat, asilimia 61 ya raia wasio na vyama na asilimia 41 ya Warepublican wanapendelea nchi yao irejee katika mapatano ya nyuklia na Iran kuliko kusalia nje ya mapatano hayo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, asilimia 47 ya watu nchini Marekani hawaamini kuwa miradi ya nyuklia ya Iran ni tishio kwa Marekani. Uchunguzi huo wa maoni umeendelea kubainisha kuwa, aghalabu ya wananchi wa Marekani wanapinga kutumiwa nguvu za kijeshi kwa ajili ya kushinikiza kusitisha uendelezaji wa miradi ya nyuklia ya Iran.
Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni matokeo ya mazungumzo makubwa ambayo hatimaye Julai 14 mwaka 2015 yalipelekea kutiwa saini mapatanoo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 yaani Russia, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani pamoja na mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya anayehusika na sera ya kigeni na masuala ya usalama. Wiki moja baadaye Baraza la Usalama la UN lilipasisha azimio nambari 231 na kuidhinisha mapatano hayo.
Serikali ya Marekani ilianza kuyakwamisha katika siku za awali za utekelezaji wake na tarehe 8 mwezi Mei mwaka 2018 Rais wa wakati huo wa nchi hiyo Donald Trump akachukua uamuzi wa upande mmoja ulio kinyume na ahadi za Washington mkabala wa mapatano ya JCPOA, na kujitoa katika mapatano hayo ya kimataifa. Trump aidha alitangaza kuirejeshea Iran vikwazo haramu vya nchi hiyo.
342/