24 Septemba 2024 - 16:21
Mohsen Rezai: Kisasi cha damu ya Ismail Haniyeh kinakuja

Mjumbe wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia jinai ya utawala wa Kizayuni ya kumuua kigaidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS hapa Tehran na kusisitiza kuwa, kisasi cha damu ya mwanamapambano huyo wa Palestina, kinakuja.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Mohsen Rezai akisema hayo katika mfululizo wake wa kuchambua sababu zinazopelekea kutokea vita na kuongeza kuwa, vita vyovyote vina mchakato wake maalumu na huanzia kwa kutoka kwenye hali ya usalama na kuingia kwenye hali ya kuzuka hitilafu na waka hitilafu zinaposhindwa kutatuliwa, ndipo ugomvi huingia kwenye hatua ya juu na kufikia hadi kuzuka vita.

Amesema kuwa, moja ya changamoto ilizo nazo Iran hivi sasa ni uhusiano wake na majirani zake wa kaskazini na kusini na kusisitiza kuwa, kuna njia na mikakati mingi ya kuepusha kutokea vita na Iran imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuzuia kutokea mapigano.

Amesema, ingawa baadhi ya wakati nchi inalazimika kuchukua msimamo laini wa kishujaa kupunguza mivutano, lakini wakati mwingine inakuwa ni lazima kuchukuliwe maamuzi makali na mazito ya kumfanya adui aogope kuendeleza chokochoko na uchokozi wake. 

Ametolea mfano wa jinai ya utawala wa Kizayuni ya kumuua kigaidi Ismail Haniyeh, mkuu wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hapa Tehran na kusema kuwa, inapofika kutokea uchokozi na jinai kama hii, hapo lazima zichukuliwe hatua za kumtia adabu adui ili aheshimu utawala wa nchi, na ndio maana kisasi cha damu ya Ismail Haniyeh kipo pale pale na kinakuja.

342/