(ABNA24.com) Kisingizio cha Washington katika uwanja huo, ni kulinda maslahi ya Marekani na kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo Ijumaa asubuhi Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani sambamba na kukariri madai yake yasiyo na msingi dhidi ya Iran alisema kuwa, Tehran ni tishio halisi kwa Washington na washirika wake katika eneo na kwamba Marekani nayo ni lazima itafanya chochote kwa ajili ya kukabiliana na nchi hii. Katika radiamali yake kufuatia matamshi ya Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Congress nchini Marekani dhidi ya kadhia ya mauzo ya silaha za Marekani kwa Saudia alisema: "Trump amesema wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni tishio halisi na Wasaudi ni washirika wetu katika kuwarejesha nyuma (Wirani). Kwa hivyo sisi tunafanya kila tunaloweza kwa ajili ya washirika wetu." Kwa msingi huo, serikali ya Trump ipo tayari kutumia mbinu mbalimbali kwa lengo la kuhalalisha mwendelezo wa mauzo ya silaha kwa utawala wa Saudia, silaha ambazo akthari yake zinatumika katika vita dhidi ya binaadamu vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya raia madhlumu wa Yemen. Trump sambamba na kuupinga kwa kutumia veto muswada wa kongresi ya Marekani uliokuwa unapinga mauzo ya silaha ya Marekani kwa Saudia na Imarati, amezitaja nchi hizo kuwa zenye nafasi muhimu katika kutekeleza siasa za Washington katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), na wakati huo huo akawakumbusha wawakilishi wa bunge hilo hususan Wademokrati kwamba, maamuzi yanayohusu usalama wa taifa kama vile mauzo ya silaha, yako mikononi mwa rais na kwamba bunge hilo halipaswi kuingilia maamuzi hayo.
Siku mbili zilizopita, rais huyo wa Marekani alipinga miswada mitatu ya Kongresi ya nchi hiyo iliyotaka kuzuiwa mauzo ya 'dharura' ya silaha za nchi hiyo kwa Saudia na Imarati ambapo alitoa sababu ya kuhalalisha hatua yake hiyo kwamba, 'Saudia ni ngome dhidi ya shughuli haribifu za Iran.' Trump ambaye mitazamo ya kibiashara ndiyo inayoainisha siasa zake za kigeni, huku akifuatilia maslahi ya kiuchumi tu kwenye mahusiano na utawala wa Saudia, amedai kuwa, kuna sababu tatu ambazo zinayafanya mauzo ya silaha kwa Saudia kuendelea. Trump ameandika kwamba: "Sababu ya kwanza na muhimu zaidi ni hii kwamba jukumu letu kuu ni kulinda usalama wa zaidi ya raia elfu 80 wa Marekani wanaoishi Saudia kutokana na mshambulizi ya Mahuthi (yaani harakati ya Answarullah ya Yemen). Pili ni kwamba muswada huo unadhoofisha utayarifu wa kijeshi wa Saudia na uwezo wake wa kulinda utawala wake wa kitaifa, kama ambavyo yana taathira hasi kwenye uwezo wa nchi hiyo (Saudia) wa kuwalinda maafisa wa kijeshi wa Marekani walioko nchini humo. Na tatu ni kwamba Saudia ni ngome muhimu mbele ya shughuli haribifu za Iran na washirika wake katika eneo."
Kwa hakika siasa za serikali ya Rais Donald Trump daima zimekuwa ni za kuunga mkono utawala wa Aal-Saud. Saudia ni mmoja wa washirika wa kistratijia na kiuchumi wa Washington katika eneo la Asia Magharibi kama ambavyo inahesabika kuwa mmoja wa wanunuzi wakubwa wa silaha za Marekani. Ni kwa ajili hiyo ndio maana serikali ya Washington haipo tayari hata kidogo kupunguza uhusiano wake na Riyadh. Wakati huo huo, katika uwanja wa siasa za kutekeleza mashinikizo zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, si tu kwamba Marekani imeiwekea vikwazo vikali Tehran ambavyo havijawahi kushuhudiwa, bali hatua ya kuongeza idadi ya askari wake katika Ghuba ya Uajemi na maji yanayolizunguka eneo hilo kwa kisingizio cha kukabiliana na vitisho vya Iran, imezidisha hali ya ukosefu wa amani na uthabiti katika eneo hili. Hivi sasa serikali ya Marekani inafanya jitihada za kuwachochea Wasaudi waendelee kuvuruga usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi. Hii ni katika hali ambayo mara kwa mara Tehran imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kutatuliwa mizozo ya eneo kupitia ushirikiano wa Iran na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi hususan Saudi Arabia. Katika uwanja huo hivi karibuni Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasilisha mapendekezo kadhaa ya kutiwa saini mkataba wa kutoshambuliana na Saudia. Kabla ya hapo pia waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran aliwasilisha mpango mwingine wa kuundwa 'Jumuiya ya Mazungumzo ya Kieneo.'
/129
source : Pars Today
Jumapili
28 Julai 2019
07:23:21
965187
Sisitizo la Pompeo kuhusu nafasi ya Saudia katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump, Marekani imezingatia sana eneo la Ghuba ya Uajemi na nchi za kusini mwa eneo hili hususan Saudi Arabia, ambapo imetiliana nayo saini mikataba ya mauzo ya silaha ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa huko nyuma.