22 Aprili 2020 - 07:30
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu; miaka 41 ya hamasa na kuzishinda njama za maadui

Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimetoa taarifa kwa mnasaba wa tarehe Pili Ordibihesht kwa kalenda ya Hijria Shamsia mwafaka na mwezi Aprili inayosadifiana na siku ya kuasisiwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kuenzi nafasi na mchango hai, ujumbe na jukumu muhimu la asasi hii ya Kimapinduzi katika kuimarisha, kulinda na kupanua Mapinduzi ya Kiislamu.

(ABNA24.com) Sehemu moja ya taarifa hiyo imeeleza bayana kwamba: Mchango na nafasi muhimu na yenye hamasa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kusukuma mbele gurudumu la Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha umri miaka 41 uliojaa baraka wa Mapinduzi ya Kiislamu imedhamini kubakia na kudumu ujumbe na fikra za Uislamu asili na kuenea kwa mapinduzi haya katika pembe mbalimbali za dunia na kushinda njama za uadui wa mabeberu wa dunia na mfumo wa Uistikbari dhidi ya taifa la Iran katika nyuga mbalimbali.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alichukua hatua iliyokuwa na upeo wa mbali kwa kutangaza rasmi kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kuasisiwa jeshi la Sepah kulikuwa chimbuko la matukio mawili makubwa.

Tukio la Kwanza: Kubadilisha mahesabu ya muqawama na kusimama kidete mkabala wa kambi ya maadui ambapo hilo lilidhihirika bayana wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tukio la Pili: Kuthibitisha nafasi muhimu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kando ya vikosi vingine vya ulinzi katika kutoa majibu kwa mahitaji ya kiusalama na kiulinzi mkabala wa harakati za vitisho.

Jeshi la Sepah lina nafasi kubwa katika mfumo wa kiulinzi uliojengeka juu ya msingi wa nguvu za kumzuia adui kuchukua hatua ya kushambulia na kutoa jibu kali kwa wavamizi. Kwa hakika asasi hii ya kiulinzi imethibitisha nafasi yake ya kistratejia na yenye kuainisha mambo katika uga wa kukabiliana na vitisho vya kiusalama na kijeshi katika mipaka ya kijiografia ya Iran ya Kiislamu.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu likilinda misingi na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limeweza kusambaratisha njama na mipango ya kishetani ya mifumo ya kibeberu na Uzayuni ikiwemo fitina ya kundi la Daesh na ugaidi wa kitakfiri na wakati huo huo, kuvifanya vitisho na hatari kuwa mbali kabisa na Iran pamoja na eneo hili kwa ujumla. Aidha jeshi la Sepah limethibitisha ustahiki wake wa kiutendaji katika uga wa ustawi wa kiulinzi na limekuwa bega kwa bega na vikosi vingine vya ulinzi hapa nchini katika kuimarisha misingi ya nguvu na uwezo wa taifa la Iran na kupiga hatua katika njia ya kuupa mafanikio mfumo wa Kiislamu hapa nchini.

Hivi sasa pia jeshi hili limekuwa na nafasi muhimu na ya kusifiwa katika mtihani mkubwa wa utoaji huduma wakati huu wa kupambana na virusi vya Corona na kuwasaidia wananchi walioathirika na mazingira ya sasa. Katika uwanja huu pia jeshi la Sepah limekuwa bega kwa bega na asasi nyingine hapa nchini na kung’ara katika uwanja huu wa utoaji huduma.

Hapana shaka kuwa, tuhuma, porojo, chuki, ugaidi na vikwazo vya Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) chimbuko lake ni nafasi muhimu na mchango hai wa jeshi hili katika kulifanya taifa la Iran kuwa na nguvu na kulinda usalama wa taifa hili mbele ya mipango michafu na ya kishetani ya mifumo ya kibeberu duniani. Taifa la Iran nalo daima limekuwa likithamini mchango, juhudi na hima kubwa ya jeshi hili lenye umahiri wa aina yake.

Meja Jenerali, Muhammad Baqiri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria Jumatatu ya jana katika kongamano la 24 la nchi nzima la Makamanda, Makamanda Wasaidizi na Maafisa wa Jeshi la Polisi Iran lililofanyika kwa njia ya video juu ya mahudhurio yaliyokuwa na hamasa kubwa ya wananchi wa Iran katika kuusindikiza mwili wa shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na mashahidi wengine na kueleza kwamba: Wananchi wa Iran wameonyesha vizuri kwamba wanawatambua maadui na wanasimama kidete mbele ya njama zao chafu dhidi ya taifa hili.

Kwa hakika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu linahesabiwa kuwa asasi iliyoundwa kutoka katika jamii na ambayo imesimama imara na kwa uwezo wake wote kukabiliana na adui ili kuonyesha nguvu na mshikamano wa taifa la Iran. Hii leo pia jeshi la Sepah likiwa na taarifa kamili juu ya matuikio ya eneo na harakati za madola yaliyotoka nje ya eneo hili, limejiandaa kikamilifu katika kila nyanja likitumia uwezo wake wa kiulinzi na wa kumzuia adui asithubutu kuanzisha shambulio; na liko tayari kukabiliana na kosa lolote lile la kimahesabu la maadui na hivyo kutoa jibu kali ambalo litamfanya adui ajute kwa kitendo chake hicho.

............
340