Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imeeleza kwamba, kutokana na tabia ya Khalifa Haftar ya kufanya hiana na kutoheshimu ahadi, serikali hiyo haikubaliani na tangazo lake la usitishaji wa upande mmoja kwani haina imani naye.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kwamba, Serikali ya Maafikiano ya Kkitaifa ya Libya itaendelea na operesheni zake halali za kijeshi za kujihami na kwamba, wakati wowote haitasita kufanya shambulio katika eneo lolote la ardhi ya Libya itakapobaini kuwa, eneo hilo ni kitovu cha tishio.

Wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar wametangaza usitishaji vita hadi mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani, tangazo ambalo limetathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa limetokana na kuzidiwa nguvu wanamgambo hao kwani katika siku za hivi karibuni wameshindwa vibaya katika medani ya vita na vikosi vya serikali inayoongozwa na Fayez al-Sarraj.
Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa kundi la wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' Jumatatu iliyopita alitangaza kupitia ujumbe wa televisheni kwamba sasa yeye ndiye mtawala wa Libya na wakati huo huo kufutilia mbali mapatano ya amani ya mwaka 2015 mashuhuri kama Mapatano ya Skhirat. Mapatano ya Skhirat yalitiwa saini mwezi Disemba 2015 katika mji wa jina hilo nchini Morocco kati ya pande mbili hasimu za Libya na kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa nchi za Kiarabu na Magharibi.
342/