Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Huo ndio wito aliotoa Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hotuba yake kwa washiriki wa kikao cha kundi la mawasiliano la viongozi wa nchi wanachama wa Harakati Isiyofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kilichofanyika jana jioni kwa njia ya mawasiliano ya intaneti. Mbali na kutilia mkazo nukta hiyo, Rais Rouhani alizitolea mwito pia nchi zote wa kushirikiana na kusaidiana kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa corona.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Dakta Rouhani aliashiria athari mbaya na haribifu za vikwazo, alivyovitaja kama hatua iliyo dhidi ya ubinadamu; na akasema: Kwa miaka kadhaa, Marekani imekuwa ikiweka vikwazo haramu na vya upande mmoja, ambavyo si tu vimewanyima na kuwakosesha haki zao wananchi wa Iran, lakini kwa hatua zake hizo imekuwa tishio pia kwa juhudi za kujenga mashirikiano baina ya pande kadhaa na ya kimataifa.
Kirusi cha corona, sasa kimegeuka kuwa janga la dunia nzima. Watu waliokumbwa na maradhi ya Covid-19 yanayosababishwa na kirusi hicho wameshapindukia milioni tatu na nusu na zaidi ya watu laki mbili na nusu wameshapoteza maisha kutokana na maradhi hayo.
Mripuko wa kirusi cha corona umeteteresha miundo ya kimataifa katika nyuga za afya, usalama, uchumi na jamii na kuhatarisha afya za watu wa mataifa ya dunia. Hata hali ya Marekani ya kuwa nchi inayoongoza kwa idadi kubwa zaidi ya vifo na maambukizo imeonyesha kuwa Washington haiwezi kutenganisha hatima na majaaliwa yake na ya jamii ya kimataifa. Endapo maambukizo ya virusi hivyo vya corona yataendelea na yatazidi kukithiri, huenda ikajitokeza hali ambayo haitaweza kutabirika. Kwa upande wa madhara ya kiuchumi pia, kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD, uwekezaji wa moja wa kwa moja wa kigeni unaotegemewa na nchi nyingi zinazoendelea utapungua kwa asilimia 5 hadi 15 katika mwaka huu wa 2020 na 2021. Kutokana na wigo mpana wa athari za janga hilo, jamii ya kimataifa inakabiliwa na uhaba mkubwa kwa ajili ya kukabiliana kwa pamoja na ugonjwa wa Covid-19. Lakini sambamba na hayo na sawa na kilivyo kirusi cha corona, hatua za ajabu zinazochukuliwa na Marekani, nazo pia zinageuka kuwa janga na balaa kwa dunia nzima. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akaeleza katika sehemu moja ya hotuba yake kuwa, kulidhoofisha Shirika la Afya Duniani (WHO) maana yake ni kudhoofisha mapambano ya pamoja ya dunia nzima dhidi ya corona. Rais Rouhani amesema: Hatua ambayo haikubaliki, ya pupa na isiyo na nadhari ya serikali ya Marekani ya kulinyima Shirika la Afya Duniani fedha linazohitaji ni kosa jengine la kistratejia la serikali hii.
Ni kama alivyoeleza pia Profesa Shireen Hunter ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha George Town mjini Washington:
"Athari za janga la corona katika mfumo wa siasa za kimataifa zitachukua muda mpaka zitakapodhihirika. Namna athari hizi zitakavyokuwa inategemea ni hatua gani nchi zitachukua katika wakati huu. Ikiwa nchi zitakuwa na ubinafsi katika uchukuaji hatua bila shaka mpasuko utakaokuja kujitokeza utakuwa mkubwa zaidi."
Ni jambo lililo wazi kwamba, Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, ambayo inaunda sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa haiwezi kupuuza na kutochukua hatua yoyote kuhusiana na suala kama hili linaloathiri hatima ya dunia nzima. Hotuba aliyotoa Rais Rouhani katika kikao cha jana kilichofanyika kwa njia ya mawasiliano ya intaneti cha kundi la mawasiliano la viongozi wa nchi wanachama wa harakati hiyo, inaweza kutathminiwa na kutafsiriwa katika muelekeo huo huo, wa kwamba, kwa upande mmoja ni indhari kwa wanaoliangalia kwa jicho la kisiasa janga linaloukabili ulimwengu mzima; na kwa upande mwingine ni mwito wa kutaka yawepo mashirikiano ya kukabiliana kwa pamoja na janga hatari la corona.../
342/