14 Juni 2020 - 08:01
Al Hashdul Shaabi yaipongeza Iran kwa msaada wake katika kupambana na ugaidi

Mkuu wa Idara ya Habari ya harakati ya wananchi wa Iraq ya al Hashdul Shaabi ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Iraq.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Muhannad al Iqabi ambaye alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 6 tangu kuasisiwa harakati hiyo amesema Iran ilisimama bega kwa bega na Iraq wakati nchi zote zilipoiacha Iraq peke yake katika jitihada zake za kupambana na makundi ya kigaidi.

Ameongeza kuwa, harakati ya al Hashdul Shaabi ni sehemu ya kikosi cha usalama cha taifa la Iraq. 

Wakati huo huo Yussuf al Kilabi ambaye ni mjumbe wa Bunge la Iraq ametoa taarifa akisema kuwa, bunge litaendelea kuiunga mkono na kuitetea harakati ya al Hashdul Shaabi na kwamba fatuwa iliyotolewa na wanazuoni wa Kiislamu ya udharura wa kuundwa harakati ya wananchi ya kupambana na makundi ya kigaidi ilikuwa nukta muhimu katika historia ya Iraq. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 13 Juni mwaka 2014 Ayatullah Ali Sistani alitoa fatua ya kuasisiwa harakati ya wananchi ya al Hashdul Shaabi kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi hususan Daesh.  


342/