Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Shirika rasmi la habari la Lebanon N.N.A liliripoti jana Ijumaa kuwa, zaidi ya askari 200 wa Israel wamejipenyeza katika mpaka baina ya Lebaon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu, karibu na eneo la Houla, kusini mwa Lebanon.
Duru za habari zimearifu kuwa, askari wa jeshi la Lebanon pamoja na Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini humo (UNIFIL) wamejiweka katika hali ya tahadhari kufuatia hatua hiyo ya kuingia askari wa Kizayuni katika eneo hilo la mpakani.
Awali, vyanzo vya habari vilikuwa vimedokeza kuwa, wanajeshi 30 wa utawala haramu wa Israel wameingia katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la al-Adisa, huko kusini mwa Lebanon.
Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab hivi karibu alikosoa vikali harakati za utawala ghasibu wa Israel zinazohujumu uhuru wa ardhi, bahari na anga ya nchi hiyo ya Kiarabu, huku akitoa mwito wa kuendelea kuwepo nchini humo kikosi cha UNIFIL.
Licha ya kupasishwa Azimio Nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya vita vya siku 33 vya Israel dhidi ya Lebanon mwaka 2006, lakini utawala huo pandikizi umeendelea kuhujumu ardhi, bahari na anga ya Lebanon.
Itakumbukuwa kuwa, tarehe 25 Mei 2000, utawala wa Kizayuni licha ya kuwa na nguvu za kijeshi, ulisalimu amri mbele ya wanamapambano wa Kiislamu wa Lebanon na ulilazimika kukimbia kwa madhila kusini mwa nchi hiyo.
342/