21 Juni 2020 - 08:04
Kuunga mkono kurefushwa vikwazo dhidi ya Iran, hatua ya Ulaya ya kutembea kwenye nyayo za Marekani

Troika ya Ulaya yaani nchi tatu za Ulaya za Uingereza Ujerumani na Ufaransa licha ya kudai zinaunga mkono mkono mapatano ya nyuklia ya JCPOA lakini vitendo vyao vinaiunga mkono Markeani ambayo imejitoa kabisa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa. Misimamo ya hivi karibuni ya troika hiyo ya Ulaya imezidi kuonesha jinsi nchi hizo tatu zisivyo na mwamana, sawa kabisa na Marekani.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, juzi Ijumaa tarehe 19 Juni zilitoa tamko hilo la pamoja na kuunga mkono waziwazi kurefushwa vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kinyume kabisa na azimio nambari 2231 lililopasisha makubaliano hayo ya kimataifa. Katika taarifa yao hiyo, nchi hizo tatu zimesema: Sisi nchi tatu za Ulaya tunaheshimu msimamo wetu kwamba kuna wajibu wa kutekelezwa kikamilifu azimio nambari 2231 lililoanza kutekelezwa mwaka 2015. Ingawa hata hivyo tunaamini kuwa  kuondolewa vikwazo vya silaha mwezi Oktoba mwaka huu kama linavyosema azimio nambari 2231 kutakuwa na madhara makubwa kwa usalama na utulivu wa kieneo.

Troika hiyo ya Ulaya imesema kwenye tamko hilo kwamba karibuni hivi nchi hizo tatu zitaomba kurefushwa vikwazo vya silaha za kawaida na teknolojia ya makombora dhidi ya Iran hadi mwaka 2023 na kwamba nchi hizo zinapanga kufanya mazungumzo na Russia na China na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanikisha lengo lao hilo. Katika tamko lao hilo, Uingereza Ufaransa na Ujerumani zimedai kuwa bado zinaheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA  na kwamba eti zitafanya juhudi zao zote kuyalinda makubliano hayo ya kimataifa lakini nchi hizo zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya kukabiliana na vikwazo vya kiwango cha juu na vya kidhulma vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran baada ya Washington kujitoa kwenye mapatano hayo. Si hayo tu, lakini nchi hizo tatu za Ulaya zimeungana na Marekani kuishinikiza Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA  na kuilazimisha kupasisha azimio la kisiasa dhidi ya Iran na wakati huo huo zimezidi kuishinikiza Tehran zikiitaka iiruhusu IAEA kukagua maeneo yake mawili ya nyuklia kwa kutegemea taarifa za uongo zilizotoka kwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Ijapokuwa nchi hizo tatu za Ulaya na hata Umoja wa Ulaya wenyewe, mara kwa mara zinadai kuwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni muhimu sana, hivyo hazitosita kufanya juhudi zozote za kuyalinda, lakini tangu Marekani ilipojitoa nchi hizo si tu zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya maana ya kutekeleza mapatano hayo, bali hata zimeamua kutumia siasa za kupoteza wakati zikiwa na matumaini kwamba mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran yatazaa matunda. Leo hii nchi za Ulaya zinapoulizwa zimechukua hatua gani ya kutekeleza kivitendo vipengee vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA zinatangaza kwa sauti kubwa kwamba zimebuni mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati yao na Iran unaojulikana kwa jina la INSTEX wakati ukweli wa mambo ni kuwa hatua hiyo ni ndogo sana katika mkabala wa utekelezaji kamili wa Iran wa mapatano ya JCPOA. 

Sasa hivi na kwa vile muda wa kuondolewa vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kwa mujibu wa azimio nambari 2231 umekaribia yaani mwezi Oktoba mwaka huu, nchi za Ulaya si tu zinafuata hatua kwa hatua nyayo za Marekani za kuishinikiza Iran, lakini hata zimeamua kuiwakilisha Washington kufanya mazungumzo na Russia na China ili nchi hizo mbili zisitumie kura zao za veto kupinga mpango wa nchi za Ulaya wa kutaka kurefushwa vikwazo dhidi ya Iran hadi mwaka 2023. 

Kusema kweli hakukosea Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran aliposema kwamba Troika ya Ulaya haina mwamana, ni sawa kabisa na Marekani.

342/