11 Julai 2020 - 10:54
Ansarullah yapinga mapendekezo ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imepinga mpango uliopendekezwa na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo, Martin Griffiths kuhusu mgogoro wa Yemen ikisema unapendelea muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Vita vya Yemen ambavyo vinaendelea kwa kipindi cha miezi 64 sasa vimeingia katika awamu ngumu na tata kuliko hapo awali. Jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi yametekeleza operesheni ya aina yake dhidi ya Saudi Arabia ambayo imesababisha hasara kubwa mno. Wakati huo huo Saudi Arabia na washirika wake wanaendeleza mashambulio yao ya kila siku ya mabomu na ndege za kivita dhidi ya taifa la Yemen. Hali hii inayoshuhudiwa katika medani za vita inaonesha kuwa, mgogoro wa Yemen hauwezi kusuluhishwa kwa mtutu wa bunduki. Wakati huo huo maambukizi ya maradhi ya aina mbalimbali vikiwemo virusi vya corona, yanazidisha hali mbaya na kutoa tahadhari kuhusu maisha ya raia wasio na hatia nchini Yemen.

Ni katika mazingira haya ndipo Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen, Martin Griffiths, akatoa mapendekezo ambayo yametambuliwa na harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah kuwa ni sawa na kucheza katika uwanja wa Saudia na washirika wake. Mpango huo wa Griffiths unajumuisha suala la kusitishwa mapigano mara moja, kutoa fursa kwa juhudi za kurejesha amani na kuacha harakati za kudhibiti maeneo zaidi ya Yemen.

Mpango huo wa Martin Griffiths umetolewa wakati Jeshi la Yemen likikaribia kutwaa eneo la Maʼrib huko katikati mwa nchi hiyo. Baada ya kukomboa mji wa al Hazm ambao ni makao makuu ya mkoa wa al Jawf, jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi yanapiga hatua kubwa kuelekea Maʼrib ambao ni mji mkuu wa kiuchumi wa Yemen na kituo kikuu cha uongozi vikosi vya muungano vamizi unoongozwa na Saudia. Eneo hilo la Maʼrib linatambuliwa kuwa na umuhimu mkubwa sana katika upande wa kiuchumi, na kudhibitiwa eneo hilo na Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen kunaweza kutatua matatizo mengi ya kiuchumi ya serikali hiyo kutokana na kuwa na rasilimali nyingi na viwanda vya mafuta na gesi na vilevile bwawa na Maʼrib na mtandao wa kilimo cha umwagiliaji.  

Harakati ya Ansarullah inaamini kuwa, mpango wa amani uliopendekezwa na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen unaweza kusitisha kasi ya kusonga mbele wapiganaji wake na jeshi la Yemen kuelekea Ma’rib, na yanaonyesha ni kwa kiasi gani afisa huyo anavyohudumia maslahi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia.

Suala hili pia limeifanya harakati ya Ansarullah itilie shaka nia ya Martin Griffiths na kuiangalia kwa jicho na wasiwasi. Hali hii ya kutokuwa na imani na mapendekezo ya Griffiths inasababishwa na kutoelewa kwake vyema hali halisi ya Yemen. Kimsingi Umoja wa Mataifa unaitambua rasmi serikali iliyojiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia na unasisitiza suala la kupokonywa silaha harakati ya wananchi ya Ansarullah inayokabiliana na wavamizi wa ardhi ya Yemen. Wakati huo huo licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kutangaza mara kwa mara kwamba, Yemen inasumbuliwa na janga kubwa zaidi la kibindamu duniani lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na umoja huo kwa ajili ya kusitisha mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen. Na baya zaidi ni kuwa, Antonio Guterres ameliondoa jina la Saudi Arabia katika orodha ya fedheha ya nchi zinazoua watoto wadogo na kukanyaga haki zao licha ya nchi hiyo kuendelea kuua watoto wa Yemen.

Sababu nyingine ya Ansarullah kukata mapendekezo ya Martin Griffiths kuhusu mgogoro wa Yemen ni mienendo mibaya ya serikali ya Saudi Arabia. Aprili mwaka huu Griffiths pia alitoa pendekezo lililokuwa na vipengee vitatu kwa ajili ya kusitisha vita nchini Yemen ambalo lilikubaliwa na pande zote mbili, yaani Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen na muungano vamizi. Wakati huo serikali ya Saudia haikuheshimu makubaliano hayo ya kusitisha vita na iliendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Yemen.

Ni kwa kutilia maanani hayo yote ndipo harakati ya Ansarullah ikasema mpango wa sasa wa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hauna nia ya kusitisha vita, bali lengo lake ni kutoa fursa kwa Saudi Arabia na washirika wake kufikia malengo yao ya kivamizi chini ya kivuli cha mpango huo.       

342/