15 Julai 2020 - 11:00
Kuendelea mgogoro wa Libya na kushadidi uingiliaji wa kigeni katika masuala ya nchi hiyo

Mgogoro wa Libya unaendelea kushuhudiwa huku nchi hiyo ikiwa imegeuzwa kuwa uwanja wa vita vya niaba baina ya mataifa mbalimbali.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Uturuki, Misri na Imarati ni nchi tatu za kigeni ambazo zimekuwa na nafasi kuu katika uga wa siasa za Libya ambapo katika siku za hivi karibuni kushadidi mapigano kumepelekea pia kuongezeka uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuwa na nafasi pana zaidi katika mgogoro huo.

Katika hali ambayo, vikosi vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa vikiwa vimejiandaa kufanya mashambulio kwa shabaha ya kukomboa mji muhimu wa Sirte, Misri imetangaza kuwa, mji huo ni mstari wake mwekundu. Rais wa Misri Jenerali Abdul-Fatah al-Sisi  ametishia kuwa, maeneo mawili ya Sirte na kituo cha jeshi la anga cha al-Jufra nchini Libya ni mstari mwekundu wa Misri na endapo vikosi vya pande mbili vitavuka mstari huo mwekundu na kusonga mbele kuelekea upande wa mashariki na kusini mwa nchi hiyo, jeshi la Misri litaingia katika nchi hiyo.

Katika uwanja huo, Jumatatu ya juzi Wabunge wa Bunge la Tobruk wakiwa wameathirika na satwa ya jenerali muasi Khalifa Haftar walitoa ruhusa rasmi kwa jeshi la Misri kutuma wanajeshi wake na kushiriki katika vita dhidi ya vikosi vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa. Hatua hiyo ilichukuliwa kwa madai ya kulinda usalama wa nchi mbili hizo.

Hata hivyo Bunge hilo halikuashiria hata kidogo uingiliaji wa madola ya Magharibi na ya Kiarabu katika masuala ya ndani ya Libya na himaya yao kwa wanamgambo wa Haftar na badala yake lilitangaza kuwa, Libya na Misri zimo katika hatari ya uingiliaji wa wazi wa Uturuki na kwamba, Cairo inahesabiwa kuwa mshirika muhimu wa kiistratejia wa Libya katika nyanja zote.

Tangu mgogoro wa Libya uliposhadidi, uingiliaji wa madola ya kigeni katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika nao uliongezeka. Uturuki iliingia rasmi katika uga wa siasa za Libya ikiiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa. Kupitia misaada ya Uturuki na vikosi vya Ankara vilivyotumwa huko Libya, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ikaweza kubadilisha karata na kuifanya hali ya mambo kuwa kwa maslahi yake.

Katika upande wa pili, himaya na uungaji mkono wa Imarati na Misri kwa wanamgambo wa Haftar ukadhihirishwa zaidi na kuongezeka. Kwa Misri na Imarati siyo tu kwamba, uwepo wao katika uwanja wa siasa na mustakabali wa kisiasa wa Misri ni jambo lenye umuhimu, bali nchi mbili hizo za Kiarabu zinafanya juhudi za kumuunga mkono Haftar ili zizuie uwepo mkubwa wa Uturuki nchini Libya. Katika uwanja huo, duru za Libya zilizoko karibu na viongozi wenye makao yao mashariki mwa Libya zimesema kuwa, Imarati imechukua hatua ya siri ya kuvipatia vikosi vya Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwana Haftar na mamluki wake ndege tano zisizo na rubani tatu zikiwa kutoka Israel.

Aidha ndege moja ya mizigo ya Imarati hivi karibuni ilitua katika kituo cha kijeshi la al-Jufra na kushusha kiwango kikubwa cha zana za kijeshi. Wakati huo huo, vikosi vya Serikali ya Kitaifa ya Libya vimetoa habari ya kujiandaa kufanya mashambulio dhidi ya mji waSirte katika siku za usoni. Sirte unahesabiwa kuwa mji muhimu na wa kiistartejia katika uga wa siasa wa Libya hivi sasa. Kabla ya hapo pia, serikali hiyo inayoongozwa na Fayez al-Sarraj ilikuwa imetangaza habari ya kuvisambaratisha vikosi vya Haftar na kutoa bishara ya ushindi. Hata hivyo maandalizi yanayoonekana sasa kwa kila upande, ni ishara ya wazi kwamba, Libya inakaribia kuingia katika vita vikubwa na vipana zaidi.

Katika mazingira haya, Umoja wa Mataifa na baadhi ya mataifa ya eneo na Ulaya yanataka kusitishwa vita na mapigano nchini Libya na kutoa fursa ya  mazungumzo mapya baina ya pande hasimu.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa sambamba na kusema kuwa, mgogoro wa Libya hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa mtutu wa bunduki ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ili mgogoro huo upatiwe ufumbuzi kupitia njia za kisiasa. Naye Heiko Mass, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani amesema, si kwa maslahi ya mtu yeyote yule kuibadilisha Libya na kuifanya kuwa Syria ya pili.

Utajiri mkubwa wa Libya hasa wa nishati ya mafuta na nafasi ya kijiografia iliyonayo nchi hiyo ambapo inajulikana kama Lango la Kuingia Afrika, ni baadhi ya mambo ambayo yamepelekea kuendelea kushuhudiwa vita baina ya mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuwania hisa katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Kwa muktadha huo inaonekana kuwa, pande zinazozozana nchini Libya zimegeuka na kuwa wawakilishi wa madola ya kigeni ynayoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Mwenendo huu umeisukuma Libya katika hatima isiyojulikana  na hata ya kugawanyika vipande vipande.

Madola ya Magharibi na majirani wa Libya nao licha ya kuwa wanazungumzia suala la kufanyika mazungumzo kwa minajili ya kufikia utatuzi na kuinasua nchi hiyo kutokana katika kinamasi ilichokwama, lakini kivitendo hayafanyi mambo yanayoonyesha kuwa, yana nia ya dhati ya kufikiwa hilo, bali yamekuwa yakichanga karata za kisiasa ili baadaye yaje kuwa na hisa katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo. Kwa mintarafu hiyo, inaonekana kuwa, katika siku zijazo Libya na mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo utakabiliwa na hali ngumu zaidi.

342/