22 Julai 2020 - 12:47
Rais Rouhani asisitiza kupanuliwa ushirikiano wa Iran na majirani pamoja na nchi rafiki

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya iran amesisitiza juu ya azma ya taifa hili ya kupanua uhusiano na ushirikiano wake na majirani zake wote pamoja na nchi rafiki.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Rouhani ametoa sisitizo hilo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri ambapo ameashiria hamu na shauku ya Iran ya kupanua uhusiano na nchi rafiki na majirani zake wote.

Rais Rouhani amesema ana matumaini uhusiano wa Iran na mataifa jirani na rafiki kama Russia, Iraq, Uturuki, Qatar, Pakistan na Afghanistan utapanuka zaidi.

Rais Rouhani ameashiria safari ya Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq hapa nchini na kusema kuwa, Tehran na Baghdad zimefikia makubaliano mazuri ya ushirikiano katika uwanja wa usafirishaji na uingizaji wa bidhaa mbalimbali baina ya nchi mbili, ushirikiano wa kiuchumi na Kibenki na kwamba, ana matumaini kwamba, makubaliano hayo yatafanyiwa kazi na kutekelezwa kivitendo.

Rais Rouhani ameashiria pia safari ya Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran huko Moscow Russia na kueleza kwamba, katika safari yake hiyo Zarif amepeleka ujumbe wa Rais wa Iran kwa Rais Vladimir Putin kuhusiana na kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa nchi hizo katika nyanja mbalimbali.

Rais Rouhani ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka na miezi ya hivi karibuni Iran imekuwa na mawasiliano na uhusiano mzuri na Russia na China ambapo katika majuma ya hivi karibuni uhusiano huo umeimarika zaidi na zaidi.

342/