Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Trump amedai kuwa, Wairani hawataki kuona ninachaguliwa tena kuwa Rais wa Marekani, wananaona bora kufikia makubaliano na Joe Biden, lakini kama mimi nitashinda urais na kuwa tena Rais wa Marekani nitafanya haraka kufikia makubaliano na Iran na hata Korea Kaskazini.
Kadhalika Rais huyo wa Marekani ambaye mara kwa mara amekuwa akitoa matamshi ya vitisho dhidi ya Iran amedai kwamba, kama Iran na China zitafikia makubaliano na Joe Biden basi mataifa hayo mawili yataimiliki Marekani.
Donald Trump anatoa madai hayo katika hali ambayo, tangu ashike hatamu za uongozi nchini Marekani ameweka mbele katika sera zake za kigeni suala la kuiwekea vikwazo na kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kama anavyodai isalimu amri na kukubaliana na matakwa ya kibeberu ya Washington.
Aidha Trump anazungumzia suala la kuhakikisha anafikia makubaliano na Iran katika hali ambayo, Mei mwaka 2018 aliitoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia na Iran yaliyofikiwa na madola makubwa ikiwemo Marekani na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa, mazungumzo yoyote ya taifa hili na Marekani yatafanyika kwa sharti Washington iachane na siasa zake za chuki na uhasama dhidi ya Tehran na katika fremu ya mazungumzo ya kundi la 5+1.
342/