Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa muda mrefu sasa Venezuela iko chini ya mashinikizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya Marekani. Viongozi wa Marekani na hasa baada ya kuingia madarakani Donald Trump, wamekuwa na msimamo wa wazi wazi na wa kivitendo wa kuipindua serikali ya Venezuela na kutaka kumuweka kwa nguvu madarakani kibaraka wao lakini hadi hivi sasa wameshindwa. Siasa hizo za kibeberu za Marekani ni kubwa kiasi kwamba viongozi wa White House hawaitambui serikali halali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Venezuela na badala yake wanadai kuwa mpinzani wa serikali hiyo, Juan Guaidó, eti ndiye rais wa Venezuela. Marekani imekuwa ikifanya njama mbalimbali zikiwemo za mapinduzi ya kijeshi, kufanya uharibifu ndani ya nchi hiyo kama kuvuruga huduma za kijamii, kuchochea magendo ya mafuta, kuifungia njia zote nchi hiyo ya Amerika ya Latini na njama na vituko vya kila namna, lakini mabeberu hao wa Marekani na vibaraka wao wameshindwa kufanikisha njama zao hizo.
Mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya Marekani dhidi ya Venezuela yanaendelea katika hali ambayo siasa hizo za kibeberu ndizo zinazoendeshwa pia na dola la kiistikbari la Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Lakini siasa hizo zimegonjwa mwamba kwani sasa hivi Marekani ndiyo iliyotengwa kimataifa na mfano wa wazi ni jinsi Washington ilivyofedheheka vibaya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kiaibu katika kampeni yake ya kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Mazingira ambayo Marekani imeziweka Iran na Venezuela yametoa fursa kwa nchi hizi mbili kushirikiana zaidi hasa katika masuala ya kiuchumi ili kukabiliana kwa pamoja na siasa za kibeberu za Washington. Ushirikiano huo ulipata nguvu zaidi baada ya Iran kuiuzia Venezuela meli tano za mafuta, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikaifikishia Venezuela meli hizo za mafuta bila ya kuogopeshwa na makeke ya Marekani iliyotishia kushambulia meli hizo. Kushindwa Marekani hata kuzisogelea meli hizo za Iran wakati zilipokuwa zinaelekea Venezuela, kulivunja kabisa majigambo ya Marekani ya kujifanya kuwa dola lenye kauli ya mwisho duniani.
Sayyid Reza Sadr al Husaini, mtaalamu wa masuala ya kimataifa amesema, kufanikiwa meli za Iran kufikisha mafuta katika fukwe za Venezuela kumesambaratisha vikwazo vya Marekani. Nchi zilizoko chini ya mashinikizo ya Marekani zinaweza kuunda umoja na muungano wao wa kukabiliana na vikwazo hivyo vya kidhalimu na kutokubali kuburuzwa na Marekani.
Sasa hivi ushirikiano wa Iran na Venezuela umeimarishwa licha ya viongozi wa Marekani kushikilia siasa zao za kuendelea kuiwekea vikwazo vya hali ya juu Venezuela. Hii ni kusema kuwa, duka kubwa la kwanza kabisa la bidhaa za Iran limefunguliwa huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela huku viongozi wa nchi hizi wakizidi kulipa umuhimu suala la kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wao bila ya kujali mashinikizo na vitisho vya Marekani. Ni vivyo hivyo, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameishukukru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake kwa wananchi na serikali ya nchi yake na kusema, Venezuela haiko peke yake, bali iko pamoja na marafiki mashujaa kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wataalamu, wanaharakati na viongozi mbalimbali duniani wanayahimiza mataifa ya dunia kutokubali kuburuzwa kiuchumi, kisiasa na kijeshi na Marekani kama ambavyo wanatilia mkazo pia wajibu wa kuungana kukabiliana na uistikbari wa dola hilo la kibeberu.
Alaakullihaal, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela, kwa mara nyingine tena ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitizia umuhimu wa kushirikiana mataifa ya dunia kukabiliana na siasa za kibeberu za Marekani. Inavyoonekana ni kwamba kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano na ushirikiano wa Iran na Venezuela kitakuwa ni kikwazo kikubwa cha kufelisha siasa za kichokozi na za kivamizi za Marekani duniani.
342/