31 Agosti 2020 - 15:16
Sayyid Raisi: Kushambuliwa Waislamu wanaoomboleza mauaji ya Imam Husain AS nchini Nigeria ni kinyume cha katiba

Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani kitendo cha wanajeshi wa Nigeria cha kuwashambulia Waislamu waliokuwa kwenye maomboleza ya Imam Husain AS na kusema kuwa kitendo hicho ni kinyume na katiba na kinakinzana na uhuru wa kila mtu kuwa na itikadi anayotaka.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hivi karibuni wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa wanaomboleza masaibu ya Karbala ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Husain AS na kuua shahidi Waislamu watatu na kujeruhi makumi ya wengine.

Sayyid Ebarahim Raisi amesema hayo leo na kukosoa pia jinsi taasisi na mashirika yanayojigamba kutetea haki za binadamu yalivyonyamazia kimya jinai hiyo. 

Amesema, kadiri maashiki na wapenzi wa Imam Husain AS wanavyoshambuliwa na kunyanyaswa, ndivyo maadhimisho ya Ashura yanavyozidi kuwa makubwa na imara.

Ameongeza kuwa, ni jambo la kushangaza kuona wanajeshi wa Nigeria wanawavamia na kuwashambulia Waislamu kwa sababu tu ya kutangaza mapenzi yao kwa Imam Husain AS, kutaja masaibu yake na kutukuza matukufu yao ya kidini.

Imam Husain AS ni Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia. Aliuawa kikatili tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Siku hiyo ilisadifiana na mwezi Oktoba mwaka 680, Milaadia. 

Jinai hiyo kubwa dhidi ya wajukuu wa Mtume wakiongozwa na Imam Husain AS na wafuasi wake, ilifanyika katika jangwa la Karbala la Iraq ya leo. Tangu mwaka huo hadi leo, maashiki na wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW wanafanya maomboleza ya kukumbuka jinai hiyo.

342/