Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Baada ya kulakiwa rasmi na mwenzake wa Iraq, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alifanya kikao cha pamoja na Rais Barham Salih wa Iraq, Waziri Mkuu Mustafa al Kadhimi na Spika wa Bunge Mohammed al-Halbousi katika ikulu ya rais wa Iraq ambacho kimejadili hali ya nchi hiyo na kanda nzima na magharibi mwa Asia.
Katika kipindi chote cha miaka 17 iliyopita hakujawahi kufanyika kikao kilichowashirikisha Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge la Iraq na rais yoyote wa nchi ya kigeni mjini Baghdad. Macron aliwasili Iraq jana Jumatano katika safari rasmi ya siku moja. Rais wa Ufaransa ambaye aliwasili Baghdad akitokea Lebanon, ametaja lengo la safari yake kuwa ni kuiunga mkono Iraq katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi. Hii ni safari ya pili ya afisa wa ngazi za juu wa Ufaransa nchini Iraq katika kipindi cha wiki moja ya hivi karibuni. Tarehe 27 Agosti Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Florence Parly alitembelea Iraq na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Baghdad na eneo la Kurdistan.
Inaonekana kuwa, kutokana na kupungua nafasi na ushawishi wa Ulaya katika masuala ya eneo la magharibi mwa Asia na kuongezeka nafasi ya Marekani na uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kijeshi ya nchi za eneo hilo, sasa nchi kubwa za Ulaya hususan Ufaransa, zimeazimia kuwa na mchango katika matukio ya eneo hilo na kudhamini maslahi yao. Mlipuko mkubwa uliotukia katika bandari ya Beirut nchini Lebanon hapo tarehe 4 mwezi uliopita wa Agosti uliitayarishia Ufaransa mazingira ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa safari mbili zilizofanywa na Rais Emmanuel Macron mjini Beirut ambako alitoa pendekezo la kufanyiwa marekebisho ya kimsingi katiba ya Lebanon.
Kwa sasa inaonekana kuwa rais kijana wa Ufaransa anataka kuwa na nafasi na ushawishi mkubwa zaidi katika eneo la magharibi mwa Asia. Macron anadhani kuwa, anaweza kutayarisha uwanja wa kupanuliwa zaidi ushawishi wa Paris nchini Iraq kwa kutoa maoni kuhusiana na masuala ya Iraq na kufanya mazungumzo ya kutaka kuwashawishi viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Baghdad.
Katika kipindi cha utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq, Ufaransa ilikuwa miongoni mwa washirika wakubwa zaidi wa utawala wa Baath wa nchi hiyo katika masuala ya kijeshi na mauzo ya silaha, na katika kipindi chote cha miaka 8 ya vita vya Saddam dhidi ya Iran, Paris ilikuwa na mchango mkubwa katika kuupa silaha utawala wa dikteta huyo wa zamani wa Iraq. Sasa Wafaransa ambao ushawishi wao wa kiuchumi na masuala ya kijeshi ya Iraq umenyauka sana kutokana na kuwepo Wamarekani nchini humo, wanataka kuzidisha nafasi yao nchini humo. Rais Macron ameashiria suala hilo katika matamshi yake pale aliposema kuwa, Iraq bado inahitaji msaada wa jamii ya kimataifa katika masuala ya ukarabati wa nchi, kuwarejesha wakimbizi na kupambana na ugaidi.
Miongoni mwa nukta muhimu zilizosisitizwa na Rais wa Ufaransa katika mazungumzo yake na viongozi wa Iraq ni udharura wa kupunguzwa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Macron amesema kuwa, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya Iraq unaidhoofisha nchi hiyo na maslahi yake ya kitaifa na kusisitiza kuwa, jambo hilo ndiyo changamoto kubwa zaidi kwa mamlaka ya Iraq.
Kama lengo la Rais wa Ufaransa pale alipozungumzia uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Iraq ni Marekani na uwepo wa majeshi ya nchi hiyo nchini Iraq ambao unadhoofisha mamlaka ya nchi hiyo na kuathiri mwenendo wake wa kisiasa, basi atakuwa amepatia na kunena kweli. Marekani licha ya kutangaza kuwa itapunguza wanajeshi wake nchini Iraq kutoka wanajeshi 5200 hadi 3500, lakini bado inaendeza jitihada za kuwa na ushawishi wa kiuchumi, kijeshi na kiusalama katika nchi hiyo.
Kwa utaratibu huo inatupasa kusema kuwa, mbali na jitihada za Emmanuel Macron za kutaka kuzidisha ushawishi wa Ufaransa nchini Iraq na kudhamini maslahi ya kiuchumi ya nchi yake katika safari yake ya sasa mjini Baghdad, lakini tunaweza kusema kuwa safari hiyo ilikuwa ya kimaonyesho tu na haiwezi kuwa na maslahi ya maana kwa nchi za Ulaya.
342/