16 Septemba 2020 - 14:21
Bunge la Taifa la Palestina: Mapatano ya Imarati, Bahrain na Israel hayatadhamini amani

Bunge la Taifa la Palestina limetangaza kuwa, kufanya mapatano na utawala haramu wa Israel kamwe hakuwezi kuleta amani, utulivu na maendeleo katika eneo la magharibi mwa Asia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa iliyotolewa jana usiku na Bunge la Taifa la Palestina imesema kuwa, baada ya kutia saini mapatano ya amani na utawala haramu wa Israel, nchi za Imarati na Bahrain zimeitambua rasmi Quds na matukufu ya Kiislamu na Kikristo ya mji huo kuwa ni mji mkuu wa Israel na kupasisha mpango wa Muamala wa Karne.

Taarifa ya Bunge la Taifa la Palestina imesema kuwa, hatari kubwa na halisi inayotishia usalama wa nchi za Kiarabu na kadhia ya Palestina ni uvamizi wa utawala wa Israel unaofanya mikakati ya kuangamiza kabisa haki za kitaifa za Palestina ikiwa ni pamoja na haki ya kurejea wakimbizi na haki ya kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu. 

Wakati huo huo mshauri wa Rais wa mamlaka ya Ndani ya Palestina Nabil Shaath amesema kuwa siku ya kusainiwa mapatano baina ya Imarati na Bahrain na utawala ghasibu wa Israel ni siku ya aibu kwa Waarabu na tawala zao, na mwendelezo wa njama za Marekani na Israel.

Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Riyad al-Maliki amesema kuwa, mapatano ya nchi hizo mbili za Kiarabu na utawala haramu wa Israel hayatasaidia propaganda za uchaguzi wa rais za Donald Trump. 

Nchi mbili ndogo za Kiarabu za Imarati na Bahrain na utawala wa Kizayuni wa Israel jana Jumanne zilisaini rasmi makubaliano hayo katika Ikulu ya White House mjini Washington, Marekani.

Makubaliano hayo ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina yamelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

342/