9 Februari 2021 - 10:43
Ayatullah Raisi: Mauaji ya shahidi Suleimani na shahidi al Muhandis hayataachwa bila ya jibu

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, jinai iliyofanywa na Marekani ya mauaji ya makamanda wa muqawama haitaachwa bila ya jibu na akabainisha kuwa, shahidi Qassem Suleimani na shahidi Abu Mahdi al Muhandis ni mashujaa wa mapambano dhidi ya ugaidi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Sayyid Ibrahim Raisi ameyasema hayo mara baada ya kuwasili mji mkuu wa Iraq, Baghdad na baada ya kuzuru eneo walipouawa shahidi kamanda Qassem Suleimani na Abu Mahdi al Muhandis na kutoa heshima zake kwa mashahidi hao wawili waheshimika wa ulimwengu wa Kiislamu.

Akihutubia katika eneo hilo lililoko karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, Ayatullah Raisi amesema, damu ya Kiirani na Kiiraqi zimeunganika pamoja katika sehemu hiyo na akasisitiza kuwa, mahali hapo ni nembo pia ya jinai za Marekani na ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, mashahidi watukufu Qassem Suleimani na Abu Mahdi al Muhandis si milki ya Iran na Iraq, bali ni milki ya umma wa Kiislamu na jamii ya wanadamu na akasisitiza kwamba, kisasi cha Mwenyezi Mungu siku zote kimelipizwa na kitaendelea kulipizwa kupitia mkono wa taifa.

Ayatullah Ibrahim Raisi ameashiria pia uungaji mkono wa Marekani kwa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) na akasema: Marekani yenyewe ndio iliyoasisi na ndio inayoliunga mkono kundi la Daesh na kulipatia kundi hilo la kigaidi suhula zote za kifedha na silaha na taarifa za intelijensia ili liteketeze roho za watu wa mataifa ya Waislamu; na mkabala na hayo inawaandama watu wanaosimama kupambana na kundi hilo.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu aliwasili mji mkuu wa Iraq Baghdad hapo jana akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa idara hiyo.

Ayatullah Raisi ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa Faiq Zaidan, mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la nchi hiyo.

Katika ziara yake hiyo ya siku tatu, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake pamoja na rais, waziri mkuu na spika wa bunge la Iraq...

342/