14 Machi 2021 - 14:20
Jeshi la Myanmar laendeleza mauaji; waandamaji wengine wanne wauawa

Waandamanaji wengine wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama nchini Myanmar huku jumuiya za kimataifa zikiendelea kutoa wito wa kusitishwa mauaji nchini humo yanayofanywa na wanajeshi waliochukua hatamu za uongozi wa nchi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Waandamanaji hao wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na vikosi vya usalama usiku wa kuamkkia leo wakati mamia ya watu walipopuuza marufuku ya kutoka nje usiku na kuwasha mishumaa kuwakumbuka wale waliouwawa tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini humo. 

Hadi sasa watu zaidi ya 70 wanaripotiwa kuuawa nchini Myanmar tangu jeshi la nchi hiyo lilipofanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi.

Maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar na kutaka kuachiliwa huru viongozi wa ngazi za juu wanaoshikiliwa kifungoni akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa yameendelea kushuuhudiwa kwa majuma kadhaa sasa.

Tarehe Mosi mwezi wa Februari jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo. Jeshi la Myanmar pia limetangaza hali ya hatari ya kipindi cha mwaka mmoja na kukomesha utawala wa kiraia uliotawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 10.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.

342/